Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri inayoifanya katika sekta ya makazi nchini. Kamati imeelekeza kufanyika kwa utafiti wa kina ili kubaini namna ya kuwezesha upatikanaji wa vifaa na teknolojia za kisasa zitakazosaidia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika.
Kamati hiyo imesisitiza kuwa ipo tayari kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na taasisi zake, ili kuhakikisha kunakuwepo na tija, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 15, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Timotheo Mzava, wakati wa kikao cha Kamati na Wizara ya Ardhi kilicholenga kuifahamu wizara pamoja na taasisi zake.
Mhe. Mzava, ambaye ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, amesema kuwa changamoto za ardhi ni nyingi, lakini Kamati itaendelea kushirikiana na Wizara ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inatatuliwa na usimamizi wa sekta unaimarika.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amewashukuru wajumbe wa Kamati kwa maoni na ushauri wao, akiahidi kuwa Wizara itayafanyia kazi kwa lengo la kupata matokeo chanya katika sekta ya ardhi na makazi.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la Nyumba la Taifa, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema Shirika litaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na ushauri wa Bunge kwa kuhakikisha linabuni na kutumia teknolojia rafiki na zenye gharama nafuu katika ujenzi wa nyumba, ili kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa Watanzania wa kipato cha chini na cha kati.
Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vinafanyika kama sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 13, unaotarajiwa kuanza Januari 27, 2026.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Kaspar Mmuya, Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga, Naibu Katibu Mkuu Bi. Lucy Kabyemera, pamoja na wajumbe wa Menejimenti na Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)


No comments:
Post a Comment