Friday, January 30, 2026

NGORONGORO SAKO KWA BAKO NA TAASISI ZA ELIMU KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII NA KUIMARISHA ELIMU YA UHIFADHI

 





Monduli, Arusha – Januari 30, 2026

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za asili na kuandaa kizazi kijacho chenye uelewa wa kina kuhusu uhifadhi endelevu, kupitia kampeni maalum ya utoaji elimu ya vivutio vya utalii na masuala ya uhifadhi kwa taasisi za elimu zilizopo Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Katika kampeni hiyo iliyofanyika leo, NCAA ilikutana na wanafunzi pamoja na walimu kutoka Shule za Sekondari Manyara, Lowasa, Rift Valley pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Mto wa Mbu, ambapo washiriki walipata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu thamani ya kipekee ya Hifadhi ya Ngorongoro, mchango wake kwa uchumi wa taifa, na wajibu wa jamii katika kuilinda kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mwakilishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro alisema kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kujenga uelewa, uzalendo na hisia za umiliki miongoni mwa vijana kuhusu rasilimali za asili, hususan vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, ambalo ni miongoni mwa maajabu ya dunia yanayotambuliwa kimataifa.

“Ngorongoro si urithi wa Tanzania pekee, bali ni urithi wa dunia. Ili uendelee kudumu, ni lazima vijana waelewe thamani yake mapema na washiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi,” alisema.

Kupitia mawasilisho, majadiliano na maswali ya wazi, wanafunzi walielimishwa kuhusu aina mbalimbali za vivutio vya utalii, ikiwemo Crater ya Ngorongoro, wanyamapori adimu, urithi wa kihistoria na kiutamaduni, pamoja na mchango wa utalii katika kuongeza mapato ya taifa na kuboresha huduma za kijamii.

Aidha, elimu ya uhifadhi iligusia masuala ya matumizi endelevu ya rasilimali, athari za uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, na umuhimu wa jamii kushirikiana na taasisi za uhifadhi katika kulinda mazingira yao.

Walimu na wanafunzi walipongeza hatua hiyo ya NCAA, wakieleza kuwa elimu waliyoipata itaongeza motisha kwa vijana kuzingatia masomo yanayohusiana na mazingira, utalii na uhifadhi, sambamba na kuwa mabalozi wazuri wa kutunza mazingira katika jamii zao.

Mwalimu mmoja kutoka Shule ya Sekondari Lowasa alisema kampeni hiyo imewawezesha wanafunzi kuona uhifadhi si dhana ya darasani pekee, bali ni jukumu la kila mwananchi.

“Hii ni elimu inayogusa maisha ya kila siku. Wanafunzi wetu sasa wanaelewa kuwa kulinda mazingira ni kulinda maisha yao ya baadaye,” alisema.

Kupitia kampeni hii, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuimarisha uhusiano wake na taasisi za elimu, ikilenga kuandaa kizazi chenye maarifa, maadili na uwajibikaji katika kulinda na kutangaza vivutio vya utalii na rasilimali za asili za Tanzania.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa NCAA wa kuwekeza katika elimu, uhamasishaji wa jamii na ushirikishwaji wa vijana kama nguzo muhimu ya uhifadhi endelevu na maendeleo ya sekta ya utalii nchini.

No comments:

  ‎
Bodi ya Kitaaluma ya Ununuzi na Ugavi (PSPTB), inayofanya kazi chini ya Wizara ya Fedha, imetoa onyo kali kwa watahiniwa wote wa fani ...