Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Subira Mgalu (Mb), imekutana na viongozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na taasisi zake, kwa lengo la kupata uelewa wa kina kuhusu muundo, majukumu na utekelezaji wa shughuli za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kikao hicho kimefanyika leo Januari 21, 2025, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, kikilenga kuimarisha usimamizi wa Bunge katika sekta ya nishati, ambayo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Subira Mgalu, amesema Kamati ina jukumu la kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinafanya kazi kwa ufanisi, kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo iliyopo, huku zikitoa huduma bora kwa wananchi. Ameeleza kuwa uelewa wa kina wa majukumu na muundo wa taasisi hizo ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kibunge na kutoa mapendekezo yenye tija kwa Serikali.
Kwa upande wao, viongozi wa Wizara ya Nishati na taasisi husika wamewasilisha taarifa zinazoeleza kwa kina majukumu ya TANESCO katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, pamoja na mchango wa REA katika kusambaza nishati vijijini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huduma za kijamii na ustawi wa wananchi.
Kikao hicho pia kimejadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya nishati, fursa zilizopo, pamoja na mikakati inayochukuliwa na Serikali kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, hususan kwa wananchi wa vijijini na maeneo yanayokua kwa kasi ya kiuchumi.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya Bunge kuendelea kusimamia kwa karibu sekta ya nishati, kwa lengo la kuhakikisha inakuwa chachu ya maendeleo endelevu, uwekezaji na kuinua maisha ya Watanzania.










No comments:
Post a Comment