Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), unaolenga kuboresha msingi wa elimu kwa watoto nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amesema mpango huo umeandaliwa kwa kutumia ushahidi wa kisayansi na uzoefu wa kitaalamu, ukiweka mkazo katika mbinu bora za ufundishaji, ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi, pamoja na kuwajengea walimu uwezo wa kitaalamu unaoendana na mahitaji ya sasa ya elimu.
Ameeleza kuwa umahiri wa kusoma, kuandika na kuhesabu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya elimu na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa watoto wanaopata msingi imara wa KKK hujifunza kwa ufanisi zaidi katika ngazi za juu za elimu na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mpango huo pia unatarajiwa kuongeza usawa wa fursa za elimu, kupunguza ufaulu duni wa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi, na kuchochea maendeleo endelevu kupitia elimu jumuishi na yenye ubora.
Mhe. Dkt. Samia, ameshiriki kucheza pamoja na kikundi cha ngoma za asili cha wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisutu mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), jijini Dar es Salaam, tarehe 29 Januari, 2026.
Uzinduzi wa mpango huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza katika elimu kwa vitendo, kwa misingi ya Kazi na Utu, ili kujenga rasilimali watu yenye maarifa, ujuzi na maadili kwa maendeleo ya Taifa.
#KaziNaUtuTunasongaMbele
#ElimuBoraKwaWote
#MaendeleoEndelevu
#Siku100ZaSamia





No comments:
Post a Comment