Na Beatus Maganja, Morogoro
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yussuf Kabange, Januari 07, 2026 aliwatunuku na kuwavisha vyeo vya uhifadhi Maafisa 84 na Askari 48 wa taasisi hiyo, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya TAWA mkoani Morogoro.
Akitoa nasaha zake kwa Maafisa na Askari hao, Kamishna Kabange aliwapongeza kwa kufikia hatua hiyo muhimu katika utumishi wa umma, huku akiwaagiza kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, nidhamu na kwa kuzingatia maadili pamoja na taratibu za kijeshi.
Aidha, Kamishna Kabange alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa Maafisa na Askari wa uhifadhi kupandishwa vyeo sambamba na utoaji wa ajira mpya.
Alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026, TAWA imepewa kibali cha kuajiri jumla ya Maafisa na Askari 550, hatua inayoongeza morali kwa wahifadhi, kupunguza changamoto za rasilimali watu, na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori pamoja na kukuza uhifadhi na utalii.
"Kwa namna ya Kipekee ninatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia Maafisa na Askari kupandishwa vyeo katika madaraja mbalimbali, kwani katika kipindi cha mwaka 2025/2026, jumla ya Maafisa 84 na Askari 48 wa Mamlaka wamepandishwa vyeo" alisema Kamishna Kabange.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Huduma za Shirika, Thabit Maarufu, licha ya kuwapongeza Maafisa na Askari waliopandishwa vyeo, aliwataka kutendea haki vyeo walivyovipata kwa kuboresha mazingira yao ya kazi, kuimarisha ushirikiano kazini, kuzingatia uadilifu na kudumisha mwenendo mzuri, mambo yatakayosaidia kufikia malengo ya taasisi na taifa kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SSP Luitiko Norman Kibanda, alisisitiza umuhimu wa weledi, nidhamu na uzingatiaji wa sheria katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa TAFORI, Wakuu wa Kanda, Maafisa Waandamizi pamoja na Askari wa TAWA.







No comments:
Post a Comment