Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
amezindua Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ambayo yanalenga kuonyesha
namna mashujaa wa Tanganyika walipambana kupata uhuru, maonyesho ambayo
yatafanyika kwa muda wa mwezi mmoja katika Makumbusho ya Taifa- Nyumba
ya Utamaduni jijini Dar es Salaam. Uzinduzi wa maonyesho hayo ambao ni
sehemu ya utekelezaji wa Mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kwa
lengo ya kuendeleza juhudi za Uhifadhi wa Hifadhi ya Urithi
Tanzania,hususani ya Ukombozi wa Afrika yanasimamiwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa maonyesho hayo, Dkt. Mwakyembe alisema mradi huo wa
kuhifadhi historia ya Ukombozi wa bara la Afrika ni muhimu kwa Tanzania
kwani unaweza kusaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini
kuliko ilivyo sasa kwani inawapa nafasi wageni ya kuona mambo tofauti na
yaliyozoeleka pindi wanapokuja nchini. Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na
Mapambano ya kupata Uhuru. “Tuna mradi ambao utatupeleka mbali sana
Watanzania, Afrika Kusini, Namibia, Angola hata wao wametuambia tusije
shangaa sehemu hiyo ikawa inaleta watalii wengi zaidi kuliko wanaokuja
kuangalia tembo na simba, urithi wa Afrika tumekabidhiwa na bara la
Afrika ni wajibu wetu Watanzania kuusukuma huu mradi maana
tumeshachelewa, Watanzania wengi labda hawaelewi mwaka 2011 kwa
kushirikiana na UNESCO tulipeleka ombi AU la mradi huu wa bara la Afrika
na wakaubariki huu mradi na wakaamua makao makuu yawe Tanzania na sisi
tukachagua Dar na hapa kitajengwa kituo kikubwa kitakuwa na historia ya
Ukombozi wa Afrika, sisi ndiyo viongozi wa huu mradi,” alisema Dkt.
Mwakyembe. Alisema ili kufanikisha mradi huo tayari wameanza kuchukua
hatua mbalimbali ili kuhakikisha pindi watakapojenga kituoambacho
kitatumika kuhifadhi vitu mbalimbali ambavyo vilitumika katika kipindi
cha ukombozi wa bara la Afrika kuwe na taarifa nyingi kuhusu bara la
Afrika. “Tunawatumia wazee walio na historia ya ukombozi wa Afrika
tumehoji zaidi ya wazee 100 na tunaendelea na hilo zoezi na tumebaini
maeneo zaidi ya 200 Tanzania ambayo yanahitaji kuhifadhiwa, ni wajibu
wangu kupeleka muswada bungeni ili tuyahifadhi na kuyalinda kwa kutumia
sheria,” alisema Waziri Mwakyembe. Balozi
wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer akizungumza
katika hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata
Uhuru. Kwa upande wa Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU),
Roeland Van de Geer alisema ni muhimu kwa bara la Afrika kuwa na
maonyesho ambayo yanaelezea historia ya bara hilo ili yatumike kuelezea
kizazi cha sasa na kijacho namna nchi za Afrika zilipambana kupata uhuru
na wao kama EU wataendelea kusaidia miradi mbalimbali yenye lengo ya
kutunza urithi wa bara la Afrika. “Ni jambo la kujivunia kwa Umoja wa
nchi za Ulaya kusaidia kufanikisha mradi huu … EU tumekuwa tukisaidia
miradi mingi na hii yote ni kwa ajili ya kutunza utamaduni na urithi wa
bara la Afrika, tumesaidia miradi mbalimbali nchini ikiwepo ya Olduvai
na Ngorongoro na tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania
kuendeleza maeneo ya kihistoria,” alisema. Afisa
Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege akizungumza katika hafla ya
uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya kupata Uhuru. Naye
Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO kanda ya Afrika Mashariki na Afisa Mwakilishi
wa Unesco Dar, Ann Therese Ndong- Jatta katika hotuba yake iliyosomwa
na Afisa Mpango Kitaifa wa UNESCO, Nancy Kaizilege alisema ni jambo zuri
kuwepo na makumbusho ambayo yanaeleza historia ya bara la Afrika na
yatawza kuwapa nafasi watu mbalimbali kutoka mataifa ya nje ya bara la
Afrika kuona na kujifunza historia ya Afrika. “Makumbusho haya ni muhimu
kwasababu ni sehemu ya ukumbusho wetu kwa baadae, kupitia makumbusho
haya tutaona historia ya bara la Afrika, historia ya mwanadamu na safari
ya kutafuta uhuru ilivyokuwa,” alisema Kaizilege. Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na
Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van de Geer
wakikata utepe katika uzinduzi wa Maonyesho ya Mashujaa na Mapambano ya
kupata Uhuru.Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa
ameongozana na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini (EU), Roeland Van
de Geer na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuangalia vitu
mbalimbali vya kihistoria ambavyo vimewekwa katikaMaonyesho ya Mashujaa
na Mapambano ya kupata Uhuru.
Comments