RC GEITA KUWAPIMA MAOFISA UGANI UWEZO WA UTENDAJI KAZI ZAO ZA KILIMO

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akimkabidhi mbegu bora ya mahindi, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi  wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa ya mbegu za mahindi, mhogo na viazi lishe uliofanyika nje ya viwanja vya ofisi ya mkoa huo jana. Kushoto ni Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo   (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhiwa mbegu hizo za mahindi zinazokabiliana na ukame  Wema.








 Ofisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, David Makabila akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Isamilo kabla ya uzinduzi wa shamba darasa la mbegu ya mahindi. Kutoka kushoto ni Mtafiti kutoka COSTECH, Dk.Beatrice Lyimo, Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti cha Maruku mkoani Kagera, Jojianas Kibula, Mtafiti Bestina Daniel na Mshauri wa Jukwaa la Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo   (OFAB), Dk.Nicholaus Nyange.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akitoa maelezo ya jinsi ya kupanda mbegu ya mahindi.
 wananchi wa Kijiji cha Isamilo wakiwa kwenye uzinduzi huo.
 Mkulima Hernick Elias wa Kijiji cha Isamilo akizungumzia changamoto za kilimo walizonazo
 Watafiti wakifanya vipimo kabla ya uzinduzi wa shamba la mbegu za mahindi katika kijiji cha Isamilo.
 Wakulima wa Kikundi cha Nguvumoja cha Kijiji cha Isamilo wakiwa shambani wakati wa uzinduzi huo.
 Mkulima wa Kijiji cha Isamilo, Salome Renatus akizungumza na waandishi wa habari.
  Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akionesha namna ya ujimbaji wa mashimo kabla ya upandaji wa mbegu za mahindi.
 Ofisa Ugani wa Kijiji cha Isamilo, Issa Pegeege, akionesha jinsi ya uwekaji mbolea kabla ya kupanda mbegu ya mahindi Wema.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari (kulia), kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akiongoza wakulima kupanda mbegu ya mahindi kwenye shamba darasa katika Kijiji cha Isamilo.
 Mkulima wa Kijiji cha Kikundi cha Nguvu moja katika Kijiji cha Kamhanga, Hamisi King akitoa maelekezo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mahindi katika kijiji hicho.
 Mtafiti kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga Kilosa mkoani Morogoro,  Ismail Ngolinda, akionesha namna ya ujimbaji wa mashimo kabla ya upandaji wa mbegu za mahindi katika Kijiji cha Isamilo. 
 Wakulima na wananchi wa Kikundi cha Kasimpya katika Kijiji cha Mnekezi kilichopo Kata ya Kaseme wakisubiri maelekezo namna ya kupanda mbegu za mahindi katika shamba darasa.
 Diwani wa Kata ya Kaseme, Andrew Kalamla akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa shamba darasa hilo.
 Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnekezi.
 Mwakilishi wa Mkoa wa Geita, Emiri Kasagala, akihutubia katika uzinduzi huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Robert Gabriel
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, akipanda mbegu wakati wa uzinduzi wa shamba darasa katika Kijiji cha Mnekezi. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Emiri Kasagala.

Na Dotto Mwaibale, Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel Lughumbi amesema ataanzisha utaratibu wa kuwapima maofisa ugani wa mkoa huo utendaji kazi wao ili kujua uwezo wa kila mmoja wao.

Hayo ameyasema  wakati Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ilipokuwa ikimkabidhi mbegu bora za mahindi, mihogo na viazi lishe ikiwa ni siku yake ya kwanza kufanya kazi katika mkoa huo tangu ateuliwe na Rais Dk.John Magufuli kushika wadhifa huo.

"Kilimo ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaingia katika uchumi wa kati wa viwanda hivyo nitaweka utaratibu wa kuwapima maofisa ugani wote wa mkoa huu ili niweze kujua utendaji kazi wao" alisema Lughumbi.

Lughumbi aliwataka maofisa ugani mkoani humo kuacha kukaa maofisi kwenye viyoyozi badala yake waende walipo wakulima kushirikiana nao kuwapa elimu ya kilimo ili kujikomboa kiuchumi kupitia kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa ameahidi kununua viatu vya shambani 'gambuti' na koti na kuwa mara moja ataanza kutembelea wakulima katika maeneo yao ili kujua changamoto zao na kusema anapenda kuona mkoa wa Geita unakuwa namba moja kwa kilimo hapa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Viumbe Hai wa COSTECH, Dk.Bakari Msangi alisema kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa na magonjwa kama batobato na ukame.

Akizungumzia mbegu bora ya viazi lishe alisema mbegu hiyo viazi vyake vinavitamini A ya kutosha ambayo ni muhimu kwa watoto na hiyo itawasaidia baadhi yao kuto kwenda Hospitali kuipata badala yake wataipata kwa kula viazi hivyo.

Msangi aliwaomba maofisa ugani pale wanapokuwa na changamoto mbalimbali za kazi yao wasisite kwenda COSTECH ili kusaidiana na kupeana mbinu mbalimbali za kilimo.

Mkulima wa Kijiji cha Isamilo, Hermick Elias alisema kukosekana kwa mbegu bora, wataalamu wa kilimo na kutofikiwa na pembejeo za kilimo kwa wakati ni moja ya sababu ambayo imewarudisha nyuma katika masuala ya kilimo lakini wanaamini kwa mbegu hizo walizoletewa na COSTECH itakuwa nu mkombozi kwao kwa kupata chakula na ziada watauza na kujipatia fedha za kuwasaidia.

Alisema kwa kilimo walichokuwa wakikifanya ekari moja walikuwa wakipata mahindi kuanzia magunia nane hadi tisa lakini kwa maelezo ya watafiti hao wa kilimo iwapo watatumia mbegu hiyo bora wataweza kupata magunia kuanzia 25 hadi 30.

Mkulima Salome Renatus aliipongeza serikali na COSTECH kwa kuwapelekea mbegu hizo hivyo wanatarajia kupata mazao yenye tija tofauti na awali.

Mbegu hizo zitapandwa katika mashamba darasa katika wilaya zote za mkoa wa Geita, Nyang'wale, Mbogwe,Chato na Bukombe.

Comments