MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MABALOZI WA UGANDA, CUBA NA IRAN KWA NYAKATI TOFAUTI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi mpya wa Uganda nchini Mhe. Richard T. Kabonero aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kujitambulisha na kufanya mazungumzo, Ikulu jijini Dar es salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja Balozi mpya wa Uganda nchini Mhe. Richard T. Kabonero mara baada ya kumaliza mazungumzo, Ikulu jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkaribisha ofisini kwake Balozi wa Cuba nchini Mhe. Lucas Domingo Hernandez . (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Balozi wa Iran nchini Mhe. Moussa Farhang aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kwa mazungumzo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia kitabu chenye historia ya miji ya Iran ambacho alikabidhiwa na Balozi wa Iran nchini Mhe. Moussa Farhang aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais kwa mazungumzo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).


…………………………………………………………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo amekutana na Mabalozi kutoka nchi tatu kwa wakati tofauti ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais alianza kwa kukutana na Balozi Mpya wa Uganda hapa nchini Mhe. Richard T. Kabonero ambaye alifika kuonana na Makamu wa Rais kwa mara ya kwanza ambapo alitumia nafasi hiyo kujitambulisha.
Katika mazungumzo na Makamu wa Rais, Balozi Kabonero alizungumzia nia ni ya dhati ya nchi yake katika kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kindugu baina ya Tanzania na Uganda hasa ushirikiano wa kijamii, na kiuchumi ambapo tafiti za mafuta zinazoendelea katika ziwa Eyasi, mashirikiano ya sekta ya anga ili kusaidia kukuza utalii, mradi wa ujenzi ya reli ya kati na mradi wa umeme vijijini pamoja na kuanzishwa kwa jukwaa la biashara la sekta binafsi kutoka nchi husika ili kuweza kunufaika na fursa zitakazojitokeza baada ya kukamilika bomba la mafuta .
Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Uganda kwa kutimiza miaka 55 ya Uhuru.Pia aliipongeza Uganda kwa kutafiti na kugundua mafuta kwa kutumia wataalamu wazawa ambapo alisisitiza ushirikiano wa kitaalamu na wataalamu wa Tanzania.


Makamu wa Rais amemtakia heri na fanaka katika majukumu mapya ya Ubalozi wa Uganda hapa Tanzania na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali.Makamu wa Rais alimalizia mazungumzo yake na Balozi huyo wa Uganda hapa nchini kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa ushirikiano wake walioutoa wakati wa ajali mbaya ya gari iliyowakuta Watanzania waliokuwa wanatoka Harusini ambapo watanzania 13 walifariki.
Wakati huohuo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe. Lucas Hernandez ambaye alisema Cuba imeendelea kuwa rafiki mzuri wa Tanzania na kushukuru sana Tanzania kuisemea Cuba iondolewe vikwazo kwenye mkutano wa 72 wa baraza kuu la usalama la umoja wa Mataifa.
Balozi huyo alisema kuna zaidi ya wataalamu 50 kutoka Cuba wapo nchini katika kusaidia katika Nyanja mbalimbali ikiwemo afya na elimu,Balozi Hernandez alisema wataalam 16 wa masuala ya afya waliwasili jana na kupangiwa kazi katika hospitali ya Muhimbili.

Cuba na Tanzania zimeendelea kuimarisha na kudumisha uhusiano uliohasisiwa na Fidel Castro na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Alisema mwisho wa mwezi huu kutakuwa na maonyesho ya biashara nchini Cuba ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara na Ujumbe wake.
Kwa upande wake Makamu wa Rais alishukuru Balozi wa Cuba kufika na kumuona na kwamba anatambua uhusiano mzuri uliopo katika nchi hizi mbili ambapo Tanzania imeendelea kufaidika na misaada ya kitaalamu kutoka Cuba haswa katika kutupatia wataalamu wa masuala ya afya, elimu ambapo pia Makamu wa Rais aliitaka Cuba kuja kutangaza vyuo vyao vya elimu ya juu kwani elimu yao haina gharama.
Makamu wa Rais aliishukuru Cuba kwa kuweza kusaidia ujenzi wa Viuatilifu kwa kuzuia malaria nchini.Katika kukuza utalii Makamu wa Rais alisema nchi hizi zinaweza kuimarisha mahusiano ya kitalii kwa kupeana ujuzi mbali mbali ambapo Cuba ni wazuri kwa Utalii wa Ufukweni.
Makamu wa Rais alisema kufunguliwa kwa Ubalozi itakuwa chachu katika kuimarisha na kudumisha uhusiano.Mwisho Makamu wa Rais alimalizia mazungumzo na Balozi wa Cuba kwa kumpongeza Rais wa Cuba Mhe. Raul Castro kwa kusimamia maono na misingi iliyoachwa na Fidel Castro.

Mwisho Makamu wa Rais alikutana na Balozi wa Iran nchini Mhe. Moussa Farhang ambaye alifikisha salaam zake kutoka kwa Makamu wa Rais wa Iran ambaye ameshukuru kwa mahusiano yaliodumu kwa miaka 40 .

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia alisema uhusiano uliopo baina ya nchi mbili hizi umegawanyika sehemu mbili ambapo moja ni uhusiano wa Kiserikali na pili ni husuniano wa kindugu ambapo mpaka leo kuna baadhi ya Vijiji, Makaburi na Misikiti inayoonyesha kuwa wa Persia waliishi Zanzibar.
Uhusiano wa Kiserikali umeendelea kuwa mkubwa katika Nyanja za kilimo na afya pamoja na kuendeleza baadhi ya programu katia vyuo vya ufundi.Makamu wa rais alisema Tanzania inaangalia namna ambavyo itarahisisha kurejesha vikao vya tume ya pamoja ya makubaliano ili kuweza kusukuma mbele maendeleo ya viwanda, Gesi na biashara.

Comments