NEEC YAFUNGUA FURSA YA WANANCHI KUMILIKI UCHUMI

Na Ismail Ngayonga.

SERIKALI ya Awamu ya Tano inaingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/17-2020/21 unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda na hivyo kufikia nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Uamuzi wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda umelenga katika kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika pato la taifa pamoja na kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira.

Ili kufikia malengo hayo juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali na mojawapo ya juhudi hizo ni kuandaa  Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NMSFEE) unaotekelezwa na Wizara na Taasisi zake; Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Sekta Binafsi pamoja na Wadau wa Maendeleo.

Utekelezaji wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unasimamiwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo ni chombo cha juu kitaifa cha kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa katika ya Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.

NMSFEE unatekelezwa kupitia Mwongozo ulioandaliwa ili kutoa maelekezo ya namna ya kutekeleza ikiwemo uratibu, usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera katika ngazi na sekta zote za kiuchumi.

Kupitia NMSFEE mfumo wa uratibu wa uwezeshaji umepangwa kwa kuwa na kamati kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji/mtaa na kila kamati ikiwa na majukumu yake kwa mtiririko endelevu. 

Mkakati wa NMSFEE imeanisha sekta mbalimbali ikiwemo mifuko ya uwezeshaji, skimu za umwagiliaji, miundombinu ya barabara, miundombinu ya masoko, huduma ya nishati vijijini, huduma za maendeleo ya biashara, hali ya biashara, urasimishaji wa ardhi, mafunzo ya ujasiriamali, na maendeleo ya vikundi vya kifedha vya kijamii. 

Katika kusimamia utekelezaji wa Mkakati huo, mwezi Julai mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua Mwongozo wa utekelezaji wa NMSFEE katika kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango na miradi mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi hapa nchini

Taarifa ya Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) inasema kuwa hadi kufikia Aprili 2017, Baraza limeweza kuendesha mafunzo kwa waratibu wa dawati la uwezeshaji wananchi kiuchumi katika halmashauri na  mikoa, maafisa mipango na Wakurugenzi wa Halmashauri.  

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo watendaji hao kufahamu wajibu na majukumu yao katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mipango ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Aidha mafunzo hayo yaliyowahusisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya yaliweza pia  yalitoa elimu kukuhusu miongozo ya kuanzisha, kuandikisha na kuendesha vikundi vya kifedha vya kijamii pamoja na Mwongozo wa ukusanyaji na utoaji wa taarifa za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Pia, waratibu wa uwezeshaji katika wizara na taasisi za Serikali wamepatiwa mafunzo hayo ili kusimamia kwa karibu utekelezaji, kuratibu, kukusanya na kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango na miradi ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika maeneo yao.

Ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchumi wa kisasa ni duni, hivyo kupitia Mkakati wa NMSFEE ni wajibu wa sekta binafsi, Serikali na wadau wa maendeleo kutoa nafasi kwa makundi yote kujiendeleza kikamilifu ili kuwajengea mazingira mazuri ya ujenzi wa uchumi imara unaoweza kuhimili ushindani katika soko la dunia.  


Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, (NEEC), Beng’ Issa.

Comments