Wednesday, March 24, 2010

Michuzi kutoa mada juu ya Blogs London


Mwasisi wa habari za jamii mtandaoni (social media) Bw. Muhidin Issa Michuzi anaondoka leo kuelekea London, Uingereza, kuhudhuria kongamano la pili la Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora 2 conference) kwa mwaliko maalumu akiwa kama blogger.

Bw. Michuzi, ambaye ametoa mchango mkubwa katika kupromoti habari za jamii mtandaoni kupitia blog yake maarufu ndani na nje ya nchi iitwayo issamichuzi.blogspot.com, amealikwa huko mkutanoni na ubalozi wetu Uingereza ili kutoa mada inayohusu umuhimu wa habari za jamii mtandaoni katika kujenga daraja kwa walio ndani na nje ya nchi.

Akiongea nasi leo kabla ya kukwaa pipa la shirika la ndege la Emirates, Bw. Michuzi ambaye pia ni maarufu kwa majina kama Mzee wa Libeneke, Mdau na Ankal, amesema amefarijika sana kuona kumbe kuna wanaotambua mchango mkubwa unaoletwa na vyombo vya habari za jamii mtandano, hasa blogs.

Amesema anajisikia mwenye furaha sana kuona azma yake ya kuifanya tasnia hii ya kupashana habari kwa njia ya intaneti kwa waandishi wa hapa nyumbani unatambulika na kukubalika na kupewa heshima stahili kama ilivyo kwa vyombo vya kawaida kama vile magazeti, redio na luninga.

Bw. Michuzi, anayeweka rekodi ya kuwa bloga wa kwanza nchini kualikwa kama bloga kwenye mkutano muhimu kama huo, anaushukuru ubalozi wetu Uingereza chini ya Balozi Mh. Mwanaidi Maajar ambaye naye anakuwa miongoni mwa wazalendo wa kwanza kuutambua hadharani mchango wa wanahabari za jamii mtandaoni kwa kutoa mwaliko huo.

"Nilijua iko siku wanahabari za jamii mtandaoni tutatambulika na mwaliko huu hakika umekuja wakati muafaka kwani msisimkmo na mwitikio wa jamii kuikubali njia hii ya mawasiliano hapa nyumbani umekuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa.

"siku hizi habari za jamii mtandaoni zinachukua kiti cha mbele katika kusomwa na wenye kuwa na intaneti kutokana sio tu na habari kuwa za uhakika, zisizochujwa na za haraka bali pia kwa kule wasomaji kupata fursa ya kuchangia habari waionayo tofauti na ilivyo kwa magazeti, redio na luninga.

"dunia imezidi kuwa kijiji kimoja kidogo kwa teknohama hii ambayo hata Rais Jakaya kikwete yuko mstari wa mbele kutaka iendelezwe mijini na vijijini ili kuwezesha wananchi wawe na habari za uhakika, za haraka na zenye kutoa fursa ya wasomaji kuchangia maoni" alisema Bw. Michuzi.

Blog ya issamichuzi.blogspot.com ilianza rasmi Septembe 8, mwaka 2005 katika jiji la Helsinki, Finland, ambako alikwenda kuhudhuria mkutano wa Helsinki Conference akiwa kama mwandishi na mpiga picha wa gazeti la Daily News.

Alikuwa ni bloga wa siku nyingi aliyekuwa anaishi Marekani wakati huo, Bw. Ndesanjo Macha, aliyemshawishi Bw. Michuzi kufungua blog yake na kuwa bloga wa kwanza wa Tanzania kuupasha ulimwengu ya kila linalojiri nchini, kazi ambayo ameifanya kwa ustadi mkubwa kiasi ni hivi majuzi tu ameweza kufikisha wasomaji milioni 8, kati ya hao asilimia 30 wakiwa ni wasomaji wa hapa hapa Tanzania.

Bw. Michuzi ameweka wazi kwamba amefurahi na kusisismkwa sio kwa sababu anakwenda ulaya, kwani ameshatembelea karibu miji mikubwa yote duniani, ukiondoa Australia na New Zealand, ila amefarijika kwa sababu hatimaye blog zimeanza kutambuliwa rasmi.

Anatoa masikitiko yake kwamba pamoja na fanaka hiyo, lakini bado hapa nyumbani jamii, hasa ya mahafidhina (conservatives) wasiotaka mabadiliko wamekuwa wazito kukubali kwamba vyombo vya habari za jamii mtandaoni vimeshapata nguvu sawa na vyombo vya kawaida kutokana na wingi wa wasomaji na hata kupelekea kujitokeza kwa wadhamini wanaotangaza biashara zao humo.

Pamoja na mambo mengine, Bw. Michuzi amesema anatamani sana kuanzisha umoja wa wanahabari za jamii mtandaoni ili kutetea na kulinda maslahi yao pamoja na kuindeleza tasnia hii ambayo inakua kwa kasi za ajabu.

Kwa mahesbu ya haraka haraka hivi sasa kuna blog zinazotumia lugha ya kiswahili zipatazo 200 ambapo pia blog takriban 10 zinaanzishwa kila siku, na kuifanya Tanzania kuw nchi zinazoendelea katika tasnia ya habari kwa njia ya mtandao.TAARIFA KWA MUJIBU WA mroki.blogspot.com

Tuesday, March 23, 2010

Mgawo wa umeme wayeyuka




HATIMAYE mgawo wa umeme ambao ulisababishwa na kuharibika kwa mitambo kwenye mabwawa manne, sasa umekwisha baada ya mafundi kufanikiwa kuirekebishwa, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema jana.
Ngeleja alisema kuwa kilichokuwa kimetokea ni hitilafu ambayo imeshafanyiwa ukarabati hivyo hali imetengemaa kwa sasa.
“Nadhani Tanesco wameshatolea maelezo hilo... mgao haupo kwa kuwa umeme wa mitambo ya Kihansi na ile nyongeza ya IPTL uko kwenye gridi ya taifa hivi sasa,” alisema Ngeleja.
Waziri Ngeleja alisema hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein kuzindua mkutano wa 28 wa sekta ya nishati kwa nchi za kusini mwa bara la Afrika (SAPP).
Ngeleja ametoa kauli hiyo wiki moja baada ya Tanesco kutangaza kuanza kwa mgao kwenye mikoa yote kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa umeme kwenye baadhi ya vituo vya uzalishaji.
Mgawo wa umeme umekuwa ukirejea kila mara licha ya Tanesco kutangaza kukomesha tatizo hilo, kutokana na uzalishaji kulingana na mahitaji na hivyo kutokuwa na akiba ya kuweza kuziba upungufu unaosababishwa na kuharibika kwa baadhi ya mitambo.
Tanesco jana walithibitisha kuisha kwa mgao huo na kuwahakikishia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwamba wataendelea kupata huduma hiyo bila bughudha.
Meneja uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema mafundi wao walikamilisha kazi ya kutengeneza mitambo iliyoharibika juzi jioni.

Alisema mitambo iliyoharibika ilikuwa katika vituo vya Kidatu mkoani Morogoro, Pangani (Tanga), Kihansi (Iringa) na Ubungo jijini Dar es Salaam.
Badra alisema kwa sasa Tanesco wana mkakati wa kumaliza tatizo sugu la upatikanaji wa nishati ya uhakika ifikapo mwaka 2032.
Akizungumzia kuhusu mkakati huo, Ngeleja alisema serikali inatarajia kutumia kiasi cha dola 11 bilioni za Kimarekani katika mpango wa muda mrefu wa kuboresha sekta ya nishati kwa muda wa miaka 25 ijayo.
Alisema kwa mpango wa muda mfupi wa kuanzia 2010-2015 serikali ina mpango wa kutumia kiasi cha dola 2 bilioni za kimarekani kuboresha sekta hiyo.
Kuhusu kupanua na kuboresha miundombinu ya sekta hiyo Ngeleja alisema serikali ina mpango wa kutumia kiasi cha dola za Marekani 7.0bilioni.
“Nishati inayopotea nchini ni asilimia 23 kutokana na miundombinu mibovu, na masuala ya kiutaalamu yamesababisha kuizidiwa kwa gridi ya taifa,” alisema Ngeleja.

SOURCE: MWANANCHI imeandikwa na Boniface Meena Zaina Malongo.

Monday, March 22, 2010

Waijua mibono kaburi



SERIKALI wilayani Kisarawe, imewahakikishia wananchi wa vijiji 11 wilayani Kisarawe ambao ardhi yao imemilikishwa kwa mwekezaji wa zao la Jatropha wilayani humo, kampuni ya Sun Biofuel ya Uingereza, watalipwa fidia zao baada ya uchambuzi yakinifu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Hanifa Karamagi, mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo, unaomilikiwa na mwekezaji huyo, ambayo inafanya mradi wa kilimo cha zao la Jatropha, au jina maarufu la mibono kaburi, kwa lengo la kuzalisha mafuta ya dizeli.

Karamagi alisema, kampuni hiyo ya uwekezaji toka nchini Uingereza, ilifuata sheria, taratibu na kanuni zote za uwekezaji na umilikaji ardhi ya vijiji kwa mujibu ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya Mwaka 1999, ikiwemo kulipa fidia stahiki kwa vijiji husika, hivyo serikali inafanya uchambuzi yakinifu kubaini kama kuna wanavijiji wowote ambao hawakupata malipo ya fidia zao kwa namna moja ama nyingine.

Karamagi pia alitoa pongezi kwa mwekezaji huyo kwa kutoa ajira rasmi zaidi ya 400 kwa wanavijiji wa vijiji vinavyozunguka mradi huo ikiwa ni pamoja na kuwalipia mafao NSSF, na kusema ajira hizo zitaboresha maisha ya wanavijiji hao, na akawasisitiza wanavijiji hao, wasibweteke na fedha za mishahara kwa kufanyia starehe, kulewa na kuongeza idadi ya wanawake, bali wazitumie fedha hizo kuboresha maisha yao na kujiletea maendeleo, ikiwemo kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula huko vijijini kwao.

Katika ziara hiyo, Mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa amefuatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kisarawe, alijionea takriban hekari 1,000 ambazo zimeshalimwa na kupandwa zao hilo, ikiwemo kushuhudia baadhi ya miche ambayo tayari imeshazaa matunda hayo ambayo mbegu zake hutumika kuzalisha mafuta ya dizeli ambayo ni rafiki wa mazingira.

Akimkaribisha mkuu wa wilaya, Meneja wa Kampuni hiyo ya Sun Biofuel nchini Tanzania, Peter Auge, alisema, kati ya ekari 8200 ambazo kampuni yake imemilikishwa, ni 6,000 tuu ndizo zitatumika kwa kwa kilimo cha mibono na eneo lililobakia litatumika kama eneo la hifadhi ya misitu asilia. Pia kampuni hiyo, itaongeza ajira toka 400 zilizopo sasa mpaka 1500 katika kipindi cha miaka mine ijayo.

Vijiji vya Mtamba, Muhaga, Marumbo, Paraka, Kidugalo, Kului, Mtakayo, Vilabwa, Mitengwe, Mzenga ‘A’ na Chakaye ndivyo wafaidika wakuu wa mradi huo, ambapo licha ya wanavijiji hao kupa ajira za moja kwa moja, kwenye mradi huo, mwekezaji huyo wa Sun Biofuel, atawajibika kuboresha huduma za jamii ukiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, na kuchangia huduma mbalimbali za maendeleo ikiwemo miradi ya afya na elimu.

Kampuni ya Sun Biofuel (T) Ltd, inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na Waingereza ambapo imejikita katika kilimo cha zao hilo la Jatropha kwa jina maarufu la Mibono Kaburi ambalo hustawi kwenye ardhi kame na isiofaa kwa kilimo cha mazao ya chakula.
SOURCE:MWANANCHI

Marekani yatoa Sh647.4 milioni BoT




SERIKALI ya Marekani imeipa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), dola 498,000 za Kimarekani (sawa na Sh647.4 milioni za Kitanzania) kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mawasiliano na teknolojia.

Fedha hizo zimetolewa na Wakala wa Biashara na Maendeleo wa Marekani (USTDA), ambayo umekuwa ikisadia nchi zinazoendelea na zenye kipato cha kati, katika masuala kama ya utafiti, mafunzo ya kibiashara na kutoa elimu ya kuwezesha kumudu miundombinu ya kisasa katika kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara.

Kutokana na umuhimu wa miundombinu ya teknolojia ya mawasiliano ya BoT, fedha hizo zitasaidia kupitia upya mfumo uliopo, sera iliyopo ya usalama, namna ya kuzifuatilia na kuzikomboa fedha zilizopotea kutokana na majanga na mipango ya maendeleo ya biashara.

Msaada huo pia utasaidia kuboresha mapitio ya kazi za kila siku za BoT.

Makubaliano ya kutolewa kwa fedha hizo yalifikiwa jana kati ya gavana wa BoT, Benno Ndulu na balozi wa Marekani nchini, Alfonso E. Lenhardt ambaye alisema fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa teknolojia ya mawasiliano ya benki hiyo.

“Msaada huu utasaidia juhudi za BoT kujiwezesha kimawasiliano na katika shughuli zake za kila siku; kuwa na uwazi pamoja na mpangilio mzuri wa bajeti,” alieleza Lenhardt.
SOURCE: UBALOZI WA MAREKANI

Chadema wafanya kufuru Dom


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Kagera, Wilfred Rwakatare, akihutubia katika mkutano wa Oparesheni Sangara, katika Uwanja wa Sabasaba mjini Kondoa mkaoni Dodoma juzi. (Mpiga Picha Wetu)

009441;
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, akihutubia katika mkutano wa Oporesheni Sangara katika Uwanja wa Sabasaba mjini Kondoa juzi. (Na Mpiga Picha Wetu)

Friday, March 19, 2010

Maaskofu wasaidizi waapishwa



Newly ordained Dar es Salaam Arch-diocese auxiliary bishops Eusebius Nzigilwa (left) and Salutarus Libena bless the Catholic faith followers and invited guests during their consecration mass at Msimbazi parish yesterday. PHOTO/SALHIM SHAO

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mamia washuhudia kuwekwa wakfu maaskofu wasaidizi
Fidelis Butahe

VIONGOZI mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa wakiongozwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa jana walihudhuria ibada ya kuwekwa wakfu, maoskofu Salutarus Libena na Eusebius Nzigilwa.

Maoskfu hao walisimikwa rasmi jana na Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, tayari kuwa wasaidizi wake katika Jimbo la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Philip Marmo aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hali kadhalika, Jaji Mkuu wa Tanzania Agustino Ramadhani, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, John Magufuli, Spika wa Bunge, Samwel Sitta, Waziri mstaafu George Kahama.

Viongozi wengine ni , Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT, Alex Malasusa.

Maaskofu hao kutoka majimbo ya Mahenge na Dar es Salaam walitangaza kuwa wasaidizi wa Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Januari 28 mwaka huu.

Hatua hiyo ilifanywa na Baba Mtakatifu Benedict wa XVI baada ya kuombwa na Kardinali Pengo, kufuatia kutokuwa na wasaidizi.

Akitoa shukrani na salamu kwa watu mbalimbali waliohudhuria ibada hiyo, Kardinali Pengo alisema Jimbo Kuu la Dar es Salaam, sasa litakuwa na wasaidizi wawili.

Alisema kwa msingi huo ameamua kuligawa katika sehemu mbili ambapo Askofu Eusebius Nzigilwa atakuwa msimamizi na mzungumzaji mkuu wa makanisa yote yaliyoko upande wa kulia wa Kanisa la Mtakatifu Joseph kuelekea mkoani Morogoro kwa kupitia Barabara ya Morogoro.

“Askofu Salutarus Libena yeye atakuwa msemaji na msimamizi mkuu wa makanisa yote yaliyopo upande wa kushoto kama unatokea kanisa la Mtakatifu Joseph kuelekea Morogoro kwa kutumia Barabara ya Morogoro”

Huku akizitaja Parokia zitakazokuwa chini ya wasaidizi wake Kardinali Pengo alisema Askofu Eusebius Nzigilwa atakuwa akisimamia Kurugenzi ya Fedha, Elimu, Afya na Caltas huku askofu Salutarus Libena akisimamia Kurugenzi ya Litulujia, Mawasiliano na Vijana.

Pia alizitaja Kurugenzi zitakazokuwa chini yake kuwa ni za Utoto Mtakatifu, Wanaume Katoliki, Wawata, Mahakama ya Kanisa, Halmashauri ya Walei Jimbo na Mapadri.

"Maaskafo hawa watakuwa na ofisi pembeni ya ofisi yangu, lakini askofu Salutarus Libena atakaa na mimi kule Kurasini na Eusebius Nzigilwa atakaa kule Osterbay kwenye nyumba ya askofu msaidizi wa zamani wa Jimbo la Dar es Salaam,” alisema.

Mara baada ya Kardinali Pengo kusoma sala wa wakfu aliwatangaza maaskofu hao rasmi na kuwapaka mafuta, kuwavalisha pete, kofia na baadaye kuwapa fimbo kama alama ya huduma ya kiuchungaji.

Hatua hiyo ilizua shangwe kutoka kwa ndugu wa maaskofu hao na kusababisha mtoa ratiba ya ibada hiyo kuwataka ndugu hao kutulia kwa kuwa ibada ilikuwa ikiendelea.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alialikwa kama mgeni rasmi kutoka serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, Philip Marmo alisema serikali inafahamu mchango wa Kanisa Katoliki si tu katika utoaji wa huduma za jamii kama elimu, afya bali hata katika upande wa kuwajenga watu kimaadili

Thursday, March 18, 2010

Tamasha la mataifa ya



Mshauri katika Ubalozi wa India hapa nchini, Ngulkham Gangte (kushoto) akifafanua jana jijini Dar es Salam katika Ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) juu ya kuanza tamasha la filamu la nchi nane za Asia ambazo ni India, China, Japan , Iran , Indonesia na Korea. Wengine wa kwanza kutoka kulia ni Mwambata wa masuala ya habari na utamaduni wa Ubalozi wa India Sanjeev Manchanda, wa pili kulia ni Mwambata wa habari na utamaduni wa Ubalozi wa Indonesia Bw.Sukamto na wa tatu kutoka kulia ni Mwambata wa masuala ya Utamaduni wa Ubalozi wa Iran Saeed Omidi. Tamasha hilo linatarajia kuanza kesho saa moja usiku katika Ukumbi wa New World Cinema na litakuwa bure. Picha na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam

RAIS SAMIA AKUTANA NA WAZEE WA MIKOA YOTE NCHINI, AFUNGUA UKURASA MPYA WA MAZUNGUMZO YA KITAIFA

  Dodoma, Agosti 27, 2025 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na wazee wa Mkoa wa Dodoma pam...