Friday, January 23, 2026
*MV NEW MWANZA YAZINDULIWA RASMI*
Thursday, January 22, 2026
MHE. NDEJEMBI AHIMIZA USHIRIKIANO WA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA NISHATI
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, leo tarehe 22 Januari, 2026, amezungumza katika Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 unaofanyika katika Ukumbi wa Mabeyo, jijini Dodoma.
Mkutano huo umeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na umewahusisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Lishe kutoka mikoa yote nchini.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Ndejembi amewasihi Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa karibu katika utekelezaji wa miradi ya nishati inayotekelezwa katika maeneo yao, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kusogeza huduma bora za nishati kwa wananchi.
WAZIRI MAVUNDE KUWACHUKULIA HATUA MAAFISA MADINI WANAOSABABISHA MIGOGORO
Dodoma | Januari 22, 2026
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao ofisi zao zitabainika kuhusika au kusababisha migogoro katika shughuli za uchimbaji wa madini, akisisitiza ulazima wa kuzingatia kikamilifu Sheria na Kanuni za Madini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Mavunde ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi kikao cha Menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Madini.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo; Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Waziri Mavunde amesema kumekuwepo na baadhi ya maafisa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.
“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo,” amesisitiza Mhe. Mavunde.
Ameagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi, ili hatua za kisheria zichukuliwe ikiwemo kuandikiwa hati za makosa na kufutiwa leseni hizo. Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Leseni kuwasilisha orodha ya kampuni zenye leseni kubwa za utafiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.
“Mimi kwa kushirikiana na Naibu Waziri tutahakikisha tunafuatilia kila leseni. Zile zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa na maeneo hayo kupewa wachimbaji wadogo wa madini,” amesema.
Kadhalika, amemtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, 2026, mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Vilevile, Waziri Mavunde amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati.
Pia amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, 2026, taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT).
Katika kuimarisha utendaji kazi, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao, akibainisha kuwa wao ndiyo taswira ya Wizara ya Madini kwa wananchi.
Wakati huo huo, Waziri Mavunde ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli kwa miaka mfululizo, akieleza kuwa makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025, mafanikio yanayotokana na maboresho ya sheria, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Hii ni hatua nzuri na nina imani kubwa kuwa tutavuka lengo lililowekwa na Serikali kabla ya Juni 30, 2026,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili Sekta ya Madini izidi kuimarika.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, wameishukuru Serikali kwa maelekezo na maboresho yanayoendelea kufanywa katika utoaji wa huduma na upatikanaji wa vitendea kazi ndani ya Tume ya Madini.
TUME YA MADINI YAFANIKISHA ZIARA YA KIKAZI KWA GHANA CHAMBER OF MINES NA GHEITI

Accra, Ghana
Tanzania kupitia Tume ya Madini imefanikiwa kufanya ziara ya kikazi kwa taasisi mbili muhimu za sekta ya madini yaani Ghana Chamber of Mines na Ghana Extractive Industries Transparency Initiative (GHEITI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi, uwazi, uwekezaji na maendeleo endelevu katika Sekta ya Madini.
Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu wa kitaalam na kujifunza kwa vitendo namna Ghana imefanikiwa kuunganisha Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika kusimamia rasilimali za madini kwa tija, uwajibikaji na maslahi mapana ya taifa. Taasisi hizo zinatambulika kimataifa kwa mchango wao katika kuimarisha sera bora, kukuza uwekezaji endelevu na kuhakikisha uwazi katika mapato yatokanayo na sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ghana Chamber of Mines amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta ya madini nchini humo. Amesisitiza kuwa sera za ushirikishwaji wa wananchi (local content) haziwezi kuleta matokeo chanya endapo hazitakuwa na msingi thabiti wa kibiashara unaoonesha manufaa ya wazi kwa pande zote zinazohusika.
“Tunaposhirikiana na Serikali, matokeo yanakuwa ya manufaa makubwa zaidi, jambo ambalo ni moja ya vipaumbele vya taasisi yetu. Ili sera za ushirikishwaji wa wananchi ziwe na maana na matokeo endelevu, ni lazima ziwe na msingi imara wa kibiashara unaoonesha faida zake kwa Serikali, wawekezaji na wananchi,” amesema.
Kwa upande wa GHEITI, ujumbe wa Tanzania umejifunza kwa kina mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya madini, ikiwemo namna taarifa za sekta ya uziduaji zinavyowekwa wazi kwa umma ili kujenga imani kwa wananchi na wadau wa maendeleo.
Ziara hiyo imewezesha Tume ya Madini kupata maarifa muhimu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa sekta ya madini, utekelezaji wa sera za uwazi, pamoja na mikakati ya kukuza uwekezaji unaozingatia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Wednesday, January 21, 2026
TANZANIA NA MAREKANI KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA MADINI
Dodoma
Serikali ya Tanzania na Marekani zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikazi katika sekta ya madini, hususan kwenye utafiti wa kina wa madini ya kimkakati yakiwemo madini ya kinywe, kwa lengo la kuimarisha usimamizi, tija, ajira na mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.
Akizungumza leo Januari 21, 2025 jijini Dodoma wakati wa kikao kilichohusisha ujumbe maalum kutoka Ubalozi wa Marekani ulioongozwa na Mhe. Andrew Lentz, Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini pamoja na wataalamu wa Wizara ya Madini, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema ushirikiano huo unatekelezwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini ya Marekani (US Department of States Enegry and Mineral Governance Program) na unalenga kuinua uwezo wa kitaifa katika utafutaji wa madini (Mineral exploration) na usimamizi wa Sekta kwa ujumla.
Aidha, Waziri Mavunde kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, ameshukuru Serikali ya Marekani ambayo kwa miongo kadhaa sasa imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia misaada mbalimbali ya kiufundi na kifedha, Mhe. Waziri amebanisha kuwa serikali ya Marekani imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania katika miradi mbalimbali inayohusu sekta za elimu, kilimo, miundombinu, afya, masuala ya utawala bora na demokrasia na mengine mengi.
Waziri Mavunde amesema kuwa misaada ya kiufundi inayotolewa na Serikali ya Marekani, ikiwemo vitendea kazi kama vishikwambi na zana nyingine za kisasa za ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za jiosayansi, ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani ya kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na hivyo kuunga mkono ajenda muhimu ya maendeleo ya nchi yetu.
Ameeleza kuwa ni wakati muafaka kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutumia fursa hiyo kikamilifu kwa kuongeza ujuzi na uwezo katika ukusanyaji, utunzaji, uchakataji na usambazajiwa taarifa za utafiti wa jiosayansi (Geo-data) kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Aidha, Waziri Mavunde amesema ushirikiano huo wa kuimarisha shughuli za utafiti za pamoja unatarajiwa kusaidia kubaini na kuibua migodi mikubwa ya madini ya kinywe katika mikoa ya Mtwara na Lindi. Hatua hii itaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya kinywe duniani. Waziri Mavunde alibainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, uhitaji wa madini ya kinywe duniani utakuwa takriban tani milioni 4.5. Hii inathibitisha uhitaji mkubwa wa madini hayo kulinganisha na hali halisi ya upatikanaji wake kwa sasa.
Vilevile, Waziri amesema kupitia ushirikiano huu wataalamu wetu wa GST na STAMICO, watapata mafunzo yatakayowajengea uwezo wa kuweza kufanya utafutaji madini kwa njia za kisasa zaidi (state of art technologies) na pia kuongeza weledi kwa ujumla katika masuala yote yanayohusu usimamizi na uendelezaji miradi ya madini.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Andrew Lentz, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano wa kikazi unaolenga matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan katika sekta ya nishati safi na salama zitokanazo na vyanzo jadidifu, kuanzia madini ya kimkakati hadi yale muhimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.
Balozi Lentz ameongeza kuwa msaada wa kiufundi unaotolewa katika eneo la utafutaji wa madini utaboresha kwa kiwango kikubwa matumizi ya mbinu nateknolojia za kisasa zaidi katika utafiti, usimamizi na uhifadhi wa taarifa a za jiosayansi, hivyo kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha tafiti za madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Yataka Uelewa wa Kina kuhusu TANESCO na REA
Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Subira Mgalu (Mb), imekutana na viongozi pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na taasisi zake, kwa lengo la kupata uelewa wa kina kuhusu muundo, majukumu na utekelezaji wa shughuli za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kikao hicho kimefanyika leo Januari 21, 2025, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, kikilenga kuimarisha usimamizi wa Bunge katika sekta ya nishati, ambayo ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Subira Mgalu, amesema Kamati ina jukumu la kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati zinafanya kazi kwa ufanisi, kwa kuzingatia sheria, sera na miongozo iliyopo, huku zikitoa huduma bora kwa wananchi. Ameeleza kuwa uelewa wa kina wa majukumu na muundo wa taasisi hizo ni msingi muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya kibunge na kutoa mapendekezo yenye tija kwa Serikali.
Kwa upande wao, viongozi wa Wizara ya Nishati na taasisi husika wamewasilisha taarifa zinazoeleza kwa kina majukumu ya TANESCO katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini, pamoja na mchango wa REA katika kusambaza nishati vijijini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi, huduma za kijamii na ustawi wa wananchi.
Kikao hicho pia kimejadili changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya nishati, fursa zilizopo, pamoja na mikakati inayochukuliwa na Serikali kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, hususan kwa wananchi wa vijijini na maeneo yanayokua kwa kasi ya kiuchumi.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya Bunge kuendelea kusimamia kwa karibu sekta ya nishati, kwa lengo la kuhakikisha inakuwa chachu ya maendeleo endelevu, uwekezaji na kuinua maisha ya Watanzania.
Tuesday, January 20, 2026
NIDA Yaaswa Kuongeza Kasi Utoaji Huduma kwa Wawekezaji
Na Mwandishi Wetu - Zanzibar
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuongeza kasi katika utoaji wa huduma kwa wawekezaji ambao wanaingia Zanzibar kwa shughuli za uwekezaji.
Ameyasema hayo Januari 19, 2026 alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za NIDA kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa, James Kaji Ikulu - Zanzibar.
Mhe. Rais amesema kuwa ameridhishwa na jitihada zinazoendelea kufanywa na NIDA za kusajili na kutambua watu, ambapo zaidi ya asilima 94 ya Wazanzibari, wameshasajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa NIDA na kupata vitambulisho ambavyo wanaendelea kufurahia matumizi ya vitambulisho hivyo.
‘’Nawataka muongeze bidii ya kuwahudumia wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza hapa Zanzibar ili kuendana na kasi ya maendeleo katika uwekezaji, kwa kufanya hivyo, itarahisisha na kusaidia kukuza uchumi kwa haraka zaidi’’ Alisema Rais Mwinyi.
Kwa upande wake Mkugugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, James Kaji amesema kuwa Ofisi za NIDA zinaendelea vizuri na kazi ya usajili na utambuzi kwa wananchi wote wanaokidhi vigezo.
Ameongeza kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inatarajia kujenga ofisi za Usajili Visiwani Zanzibar katika Wilaya za Magharibi A, Micheweni na Kusini, pamoja na kufungua ofisi ndogo katika eneo la Tumbatu - Unguja na Kojani - Pemba ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuongeza kasi ya usajili.
Akihitimisha taarifa yake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha NIDA kupata fedha kwa ajili ya kununua magari 145 ambayo kwa kiasi kikubwa yatarahisisha shughuli za usajili na utambuzi wa watu Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa Ushirikiano na kuiwezesha Ofisi ya Uratibu NIDA Zanzibari kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya msingi ya Usajili na Utambuzi Watu.
*MV NEW MWANZA YAZINDULIWA RASMI*
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezindua meli ya kisasa MV New Mwanza, akibainisha kuwa ni uwekezaji wa kimkakati wa Serikali katika kui...
-
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu na timu ya Wakurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ...
-
Mwanamuziki toka Jamhuri ya KIdemokrasia ya Kongo, Mbilia Bel akitumbuiza katika viwanja vya bunge mjini Dodoma jana. Picha na Jube Tranquil...
-
Hapa mmoja wa watoto hao akiwa na kijana mwenzake mwenye miaka 18, wote wako sawa lakini yeye hawezi kuzungumza kama watu wa kawaida. Mama S...

















































