Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) tarehe 16 Desemba, 2024 amewasili jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 16 hadi 18 Desemba, 2024 na kupokelewa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo katika ofisi za ubalozi huo.
Baada ya kuwasili Mhe. Kombo alifanya kikao kazi na watumishi wa Ubalozi huo pamoja na Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri (JMC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Desemba, 2024 jijini Addis Ababa.
Waziri Kombo anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo wa JMC akiwa ameambatana na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb.) ambapo pamoja na masuala mengine mkutano huo unatarajiwa kujadili utekelezaji wa maeneo mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa na nchi hizo mbili ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama, diplomasia, afya, maji, elimu, fedha, mifugo na uvuvi, kilimo, biashara na uwekezaji, viwanda, nishati, ushiririkiano katika sekta ya anga na michezo, Sanaa na utamaduni.
Mkutano wa Mawaziri ulitanguliwa na Mkutano wa ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika tarehe 16 Desemba, 2024 ambapo ulikuwa na jukumu la kupitia nyaraka mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo muhimu wenye lengo la kukuza ushirikiano wa kimaendeleo kwa maslahi ya pande zote mbili
Comments