UNESCO YARIDHISHWA NA HIFADHI YA JIOLOJIA YA NGORONGORO LENGAI





Na Kassim Nyaki, NCAA.

Kikao cha Wajumbe wa Baraza la UNESCO la Jiopaki kilichofanyika tarehe 10 Desemba, 2024 kwa njia ya mtandao kimeridhishwa na shughuli za uhifadhi wa Jiolojia ya Ngorongoro Lengai ambapo NCAA imewakilishwa na Afisa Uhifadhi Mkuu Dkt. Agness Gidna.

Tanzania kupitia Jiopaki pekee iliyoko kusini mwa jangwa la Sahara ya Ngorongoro-Lengai (Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark) ambayo inatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imepata kadi ya kijani (GREEN CARD) kama ishara ya umahiri katika uhifadhi na utangazaji wa eneo lenye hadhi ya hifadhi ya Jiolojia (Geopark) kwa kufuata masharti na miongozo ya UNESCO.  

Kwa utaratibu wa UNESCO, maeneo yenye hadhi za Jiolojia (Geopark) za UNESCO zinakaguliwa kwa kina kila baada ya miaka minne kwa ajili ya kupima na kuona  ufanisi na ubora kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa na UNESCO. 

Hifadhi ya Jiolojia ya Ngorongoro Lengai (Geopark) inayosimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongroro ilipata hadhi ya kutambuliwa na UNESCO Global Geoparks mwaka 2018, kutambuliwa huko kuliifanya kuwa Jiopaki pekee kusini mwa jangwa la Sahara na jiopaki ya pili katika bara la Afrika ikitanguliwa na M'Goun geopark ya nchini Morocco. 

Katika tathmini na ukaguzi uliofanywa  na wataalam kutoka UNESCO mwaka 2022, hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro Lengai ilipata kadi ya njano (Yellow Card), ambapo kwa miongozo ya UNESCO Ngorongoro Lengai ilitakiwa kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ndani ya miaka miwili ili kulinda hadhi iliyopewa mwaka 2018.

Jitihada za serikali kupitia NCAA hasa katika uimarishaji wa shughuli za uhifadhi, Ulinzi, kutangaza, kufuata masharti na miongozo ya UNESCO katika kulinda hadhi ya eneo hilo ili kuendelea kuwa Hifadhi ya Jiolojia inayotambulika kama “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” zilizaa matunda baada ya timu ya UNESCO iliyokuja mwezi julai, 2024 kufanya uthibitishaji upya (Revalidation) ambapo waliridhika na hatua zilizofanywa na Serikali katika kufuata ,miongozo ya UNESCO katika eneo hilo.

Faida ambazo Tanzania itazipata kwa kuwa na kadi ya kijani (GREEN CARD) ni pamoja na kuongezeka kwa muonekano chanya wa uhifadhi kwa nchi ya Tanzania kimataifa, kuongezeka kwa idadi ya watalii na watafiti watakaotembelea nchi ya Tanzania kwa Shughuli mbalimbali.

Faida zingine ambazo nchi inazipata ni pamoja na kupanua wigo wa mashirikiano ya kimataifa katika sekta ya uhifadhi na utalii wa hifadhi ya Jiolojia (Geopark) pamoja na kuongeza fursa ya kuongeza vivutio vingi vya utalii na hasa utalii wa miamba.

Comments