RAIS SAMIA NI KIONGOZI ANAYECHUKIA RUSHWA KWA VITENDO : NAIBU WAZIRI MHE. SANGU


Na. Lusungu Helela – Arusha.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyejipambanua kwa vitendo kwa kuichukia rushwa ambapo katika Uongozi wake ameiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) rasilimali fedha pamoja na watumishi.

Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo Desemba 18, 2024 jijini Arusha wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Philip Mpango akimwakilisha Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka 2024 wa Viongozi wa TAKUKURU.

Amesema Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu ameipaTAKUKURU vibali vya kuajiri jumla ya watumishi wapya wapatao 980 ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aidha, Mhe.Sangu amesema TAKUKURU imewezeshwa rasilimali fedha na vitendea kazi ikiwamo magari, samani na kompyuta pamoja na kujipatia fedha za ujenzi wa majengo ya ofisi katika wilaya, mikoa na jengo la makao makuu ya TAKUKURU.

Amesema uwezeshaji huo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambapo umeimarisha utendaji kazi wa TAKUKURU na kuongeza ufanisi kwenye mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu ameiagiza TAKUKURU kujipanga vyema kudhibiti vitendo vya rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025 ili kupata viongozi watakaowaletea wananchi maendeleo.

Amesema viongozi watakaochaguliwa kwa rushwa hawawezi kukemea rushwa hadharani na wala kuwaletea wananchi maendeleo

”Rushwa ni adui wa maendeleo na tukiacha vitendo vya rushwa vitamalaki katika uchaguzi tutapata viongozi wasiokuwa waadilifu na malengo ya Serikali ya kuleta ustawi wa wananchi hayatafanikiwa,” amesisitiza Mhe.Sangu

Hata hivyo Mhe.Sangu ametoa rai kwa jamii kutokukubali kushiriki vitendo vya rushwa katika uchaguzi ujao huku akiitaka jamii kushiriki kikamilifu kwenye kufanikisha uchaguzi unakuwa wa huru na haki.

”Kila mmoja wetu akikataa kushiriki vitendo vya rushwa tutakuwa tumeshiriki kuijenga Tanzania yenye maendeleo ” amesema Mhe.Sangu.






 

Comments