Mazizini, Zanzibar – Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, leo ameweka Jiwe la Msingi kwa Barabara ya Mazizini, Chukwani, na Maungani yenye urefu wa kilomita 28.164, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Mradi huu wa barabara unalenga kuboresha miundombinu, kukuza uchumi wa wananchi, na kurahisisha huduma za usafirishaji katika maeneo haya. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema kuwa hatua hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia maendeleo ya miundombinu.
"Barabara hii itakuwa kiungo muhimu kwa wakazi wa Mazizini, Chukwani, na Maungani, na itafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya Zanzibar nzima," alisema Mheshimiwa Hemed.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda miundombinu hiyo mara itakapokamilika ili iweze kudumu na kutimiza malengo yake.
Sherehe hizi ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu, yaliyotoa mwelekeo mpya kwa maendeleo ya Zanzibar.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
28 Desemba 2024
No comments:
Post a Comment