Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda, amesema kuwa imani yake kwa Mungu imemsaidia kuvuka kipindi kigumu maishani mwake.
Akizungumza jana kwenye misa ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na kumkumbuka baba mzazi wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, iliyofanyika Nyakabindi, Bariadi, Dkt. Nawanda alieleza kuwa changamoto za maisha ni mitihani ya imani na uvumilivu.
“Nimepitia kipindi kigumu sana, lakini Mungu humpatia mtu mtihani ambao anajua anaweza kuushinda. Leo, kwa nguvu za Mungu, naweza kusema nimefanikiwa kushinda,” alisema Dkt. Nawanda.
Katika hotuba yake, aliongeza kuwa kesi iliyokuwa ikimkabili ilimfundisha thamani ya kuishi kwa amani na kushirikiana na watu. Alitoa shukrani za pekee kwa wananchi wa Simiyu kwa mapenzi na maombi yao yaliyompa nguvu wakati wa changamoto hiyo.
Ikumbukwe kuwa mnamo Novemba 20, 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu ilimwachia huru Dkt. Nawanda baada ya kutomkuta na hatia katika kesi ya kulawiti iliyokuwa inamkabili.
Dkt. Nawanda alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kumtumainia Mungu na msaada wa jamii katika kushinda changamoto za maisha, akiwataka watu wote waendelee kuwa na imani na mshikamano.
Comments