Benki ya CRDB yafungua matawi mapya Mugango, Sirari mkoani Mara
Katika
kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi
mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma
Vijijini na Sirari wilayani Tarime.
Afisa
Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa
matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya
‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa
huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa
taifa pia.
“Mkoa
wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na
machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu
kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi
katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha
tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema
Raballa.
Kabla
ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo
hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa
maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao
zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime
na 35 Musoma Vijijini.
“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa.
Kutokana
na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla
ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti,
Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na
mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote
nchini.
Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.
“Tawi
hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni
mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu
na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa
kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili
kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema
Mheshimiwa Gowele.
Licha
ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza
wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa
ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond
inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha
ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA).
“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele.
Kwenye
uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald
Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na
huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu
ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake.
“Ufunguzi
wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba
wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia
kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna
bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,”
amesema Kusaya.
Sambamba
na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi
madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha
mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo
yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba
uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime.
Comments