…….
Na Mwandishi Wetu,Tanga
KATIBU wa Halmashauri Kuu(NEC)Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Issa Gavu ameitaka Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT)kuongeza kasi ya kuongeza wanachama wake na kufikia Milioni tisa kutoka wanachama Milioni 6.1 walioko sasa.
Mbali na kuongeza wanachama kwa Jumuiya hiyo ametumia nafasi hiyo kutoa maelekezo kwa wale wote ambao wanataka kushirikiana na Chama na Jumuiya zake basi wafuate maelekezo na muongozo wa Chama na kusisitiza katika Chama hicho hakuna mkubwa na maamuzi yote yanatolewa kupitia vikao vya Chama hicho.
Akizungumza Desemba 15,2024 katika Mkutano wa Baraza la Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT) Gavu aliyekuwa amemwakilisha Katibu Mkuu Dk.Emmanuel Nchimbi ,amesema amefurahishwa na taarifa ya mafanikio yaliyoelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Marry Chatanda yakiwemo ya kuongeza wanachama wapya.
“Naamini hii ni chachu katika safari ya kutafuta ushindi wa Chama chetu kwa mwaka 2025 ,nawapongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuingia kwenu madarakani .Katika taarifa yenu mmeonesha idadi kubwa ya wanachama wapya walioingizwa katika Jumuiya hiyo kutoka wanachama Milioni 4.1 mpaka wanachama Milioni 6.1.
“Maana yake kuna wanachama takribani milioni mbili na hili mmelifanya katika kipindi cha miezi 12, hongereni sana.Katika hili tuendelee kuongeza kasi ya usajili na kuhimiza wanachama wapya wajiunge na Jumuiya yetu hivyo hivyo wajiunge na Chama chetu kwasababu hatuna mtaji mwingine wa kufafutatia ushindi wa Chama zaidi ya wanachama,mashabiki na wapenzi wa Chama chetu pamoja na wanachama na wapenzi wa Jumuiya zetu,”amesema Gavu.
Ameongeza kuwa wakiendelea kusajili wanachama wapya maaana yake watakuwa wameongeza mtaji wa ushindi wa Chama cha Mapinduzi, hivyo amemuomba Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na viongozi wengine wa jumuiya hiyo kuongeza kasi zaidi.
“Kasi yenu ya kutoka Milioni 4.1 mpaka Milioni 6.1 ni kasi nzuri lakini tujitahidi kuongeza kasi ili malengo tuliyoweka sisi katika Chama chetu ya kufikisha wanachama Milioni 12 mwaka huu basi nanyi mjivute mpaka kufika wanachama Milioni 9 mwisho wa mwaka huu
“Kwahiyo ninachokiomba tuendeleze jitihada hizi za kuongeza wanachama katika Jumuiya zetu na kama Mwenyekiti tunafikiria vizuri na kuwaza vizuri yapo mambo yanatuonesha kwa kiasi gani mafanikio haya yanatokana na Chama chetu,yanatokana na Jumuiya zetu.”
Akieleza zaidi Gavu amesema hivi karibuni wamemaliza uchaguzi wa Serikali za Mitaa lakini kabla ya uchaguzi huo kulikuwa na taasisi nyingi nje ya Mfumo wa Chama chao ambazo zilikuwa zinajinasibu na kujisifia kuwa wao ndio walikuwa wanafanya kazi ya kumsaidia Rais,kumsifia Rais , kumtangaza Rais lakini ulipofika wakati uchaguzi huo waliosimama kwa ajili ya kukinadi Chama hicho ni wao wenyewe.
“Hakuna taasisi ,hakuna chawa,hakuna kunguni bali tuliokwenda kwenda kusimama,kukinadi na kukipigania Chama chetu tulikuwa ni sisi wana CCM na Jumuiya zetu.Kwahiyo Mwenyekiti wa Jumuiya UWT nataka msimame kwa miguu miwilii
“Mjipige kifua na muwathibitishie watanzania kwamba Chama chetu hakina shida ya watu wa kupiga debe , Chama chetu kipo kamilifu kina muundo thabiti, Jumuiya na wanachama tathibiti na sisi tumeamua kama tulivyoshinda katika Serikali za Mitaa,ushindi huo huo tutashinda katika uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
“Tunachokiomba wale wanachama,mashabiki na wapenzi wanaohitaji kutengeneza taasisi ama Vikundi au mikusanyiko yao kwa ajili ya kutusaidia kazi wasikilize miongozo na taratibu zitakazotolewa na Chama Cha Mapinduzi.
“Hatutoruhusu wala hatutokubali atokee mtu binafsi awe yeye msemaji wa Chama chetu,awe yeye msemaji wa Rais wetu,awe yeye mpambanaji wa maslahi ya nchi.Tutaendelea kuwahimiza na kuwakumbusha kushirikiana na mtu,kusaidiwa na mtu ama kuambatana na mtu lakini anayehitaji kutuchangia,kutusaidia na kushirikiana nasi lazıma afuate miongozo na maelekezo yanayotokana na Chama chetu,”amesema Gavu.
Amefafanua kuwa ameyaeleza hayo kwasababu wako baadhi ya watu wanakwenda katika jumuiya hiyo kuwababaisha kwa kuwaambia wametumwa na wakubwa,hivyo amesisitiza Chama chao hakina mkubwa na uamuzi wa Chama unafikiwa katika uamuzi wa vikao na vikao vyetu viko vitatu
“Tunakikao cha Mkutano Mkuu,Halmashauri Kuu na Kamati Kuu na katika vikao vyote hivyo vitatu hakuna mtu aliyebarikiwa kwenda kutuharibia chama chetu na Mfumo unaotupa heshima mbele ya jamii, hivyo nitumie nafasi hii niwaombe endeleeni kubaki katika mstari wenu ,pambanieni Chama chenu ,pambanieni Jumuiya yetu.
Comments