Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akisaini kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama An Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion. na Serikali ya Kisultan ya Oman, ikiwakilishwa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi. Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Kodi, Mjini Muscat nchini Oman na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha-Tanzania, Bw. Elias Kalist na kwa upande wa Oman, alikuwepo Mtaalam wa masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Bi. Salwa Khalfan Eid-Al-salti. Mhe. Waziri Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi nchini Oman.
Na Benny Mwaipaja, Oman
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman,
zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na
Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama Agreement for the Elimination of
Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax
Avoidance and Evasion.
Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut nchini
Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck
Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser
Al-Jashmi.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba
huo ni hatua muhimu katika jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kufungua uchumi wa
nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.
Ameongeza kuwa Mkataba
huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya
Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara
mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi
wa biashara kwa pande zote mbili.
Mkataba huo pia unalenga
kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hususan
kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sambamba na
wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia
kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na
kuongezeka kwa ajira kwa wananchi.
Aidha, wawekezaji wa
Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku
wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili.
Hatua
hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli
zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.
Kwa
ujumla, Mheshimiwa Dkt. Nchemba amesema kuwa mkataba huo unatarajiwa
kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na
Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania
kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi, na
mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika
Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akibadilishana Hati ya Mkataba na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Bw. Nasser Al-Jashmi. Mkataba unaohusu makubaliano ya Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama An Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion. Kati ya Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, Tukio hilo limefanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Kodi, Mjini Muscat nchini Oman, ambapo Mhe. Waziri Dkt. Nchemba yuko katika ziara ya kikazi nchini humo.
(Pich ana Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-Muscat-Oman)
Comments