Ni Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya siasa ya Mkoa ya CCM Mjini pamoja na Wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho wakimsikiliza kwa Umakini Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima huko Katika Ukumbi wa CCM Amani Unguja.
Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni CCM Taifa,Nd. Pereira Ame Silima akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya siasa ya Mkoa ya CCM Mjini pamoja na Wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho huko Katika Ukumbi wa CCM Amani Unguja.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU wa NEC, Idara ya Organazesheni ya CCM Taifa, Nd. Pereira Ame Silima amewataka viongozi na watendaji wanaochaguliwa kwenye uchaguzi wa chama na jumuiya zake kwa sasa kuwa na fikra na mitizamo mipya itakayoongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya CCM.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa za Mikoa ya CCM Mjini na Magharibi pamoja na wajumbe wa sekreterieti na kamati Tekelezaji za jumuiya za Chama hicho huko Amani Unguja, alisema chama hicho kitaendelea kuwa imara kutokana na utamaduni wa kupata viongozi kwa njia za kidemokrasia hasa Uchaguzi huru na wa haki.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha chama sambamba na kujitambulisha kwa viongozi hao kwani tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni Mjini Dodoma hiyo ndio ziara yake ya mwanzo.
Alizitaka kamati mbali mbali zilizopewa dhamana ya kusimamia na kuchuja viongozi katika uchaguzi wa chama hicho kuhakikisha wanapatikana viongozi wenye nia ya kweli ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji ndani ya chama hicho na sio wababaishaji.
Aidha Katibu huyo alisema Chama hicho kina nia ya kuanzisha utaratibu wa kutengeneza kadi za uanachama zitakazokuwa katika mfumo wa kielectroniki ili kupata idadi kamili ya wanachama kwa lengo la kujipanga katika michakato ya uchaguzi wa ndani na wa Dola.
“ Viongozi na watendaji wenzangu tujue kuwa chama cha mapinduzi kipo kwa ajili ya wananchi wote hivyo lazima tufanye kazi kwa ushirikiano ili tutimize kwa vitendo dhamira ya mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Katiba yanayolenga kuongeza ufanisi katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiuchumi ndani ya chama chetu.”, alisema Katibu Amen a kuongeza kuwa dhana ya CCM mpya itekelezwe na kusimamiwa na fikra mpya na sio upya wa viongozi wanaochaguliwa kwa sasa.
Alisisitiza umuhimu wa kufuata Katiba kwa kila hatua ya kufanya maamuzi ndani ya chama hicho kwa lengo la kupunguza malalamiko yasiyokuwa ya lazima kwa baadhi ya wanachama wanaokwenda kinyume na maadili ya Chama hicho.
Hata hivyo aliyataja majukumu muhimu yanayotakiwa kutekelezwa na idara yake kuwa ni kusimamia Uchaguzi wa Chama na Dola pamoja na kusimamia jumuiya za CCM kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa miongozo ya Kikatiba.
Mapema akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Bora Afya Silima Juma alisema Mkoa huo unaendelea kupanga mikakati ya kudumu itakayosaidia chama hicho kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Akisoma taarifa ya utekelezaji Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi, Aziza Ramadhan Mapuri alisema licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo katika uchaguzi unaoendea hivi sasa ndani ya mkoa huo wamefanikiwa kuwapata viongozi makini na wachapaka kwa baadhi ya ngazi ambazo tayari zimeshakamilisha zoezi hilo.
Comments