HAKIKISHENI MTWARA INAPATA MAJI KWA ASILIMIA 100 – PROF. MKUMBO


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akipokea maelezo kutoka kwa Mkuregenzi Mtendaji wa Mamlaka ya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA), Inj. Mashaka Sitta alipotembelea chanzo cha maji cha Mtawanya, mkoani Mtwara pamoja na Inj. Najib Asumbwile kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwa kwenye Mtambo wa Maji wa Kusafishia Maji, mkoani Mtwara.
 Sehemu ya Mtambo wa Kusafishia Maji, mkoani Mtwara.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akikagua sehemu ya majengo mapya ya Ofisi za Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini ambayo ujenzi wake unaendelea, akiwa na Afisa Bonde, Msiru Msengi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza kwenye ofisi ya Katibu Tawala Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoa wa Mtwara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA) ifanye bidii na kuhakikisha Mtwara inapata maji kwa asilimia 100, ikizingatiwa ni mji ulio na viwanda vikubwa, ili kuunga mkono Sera ya Viwanda inayotekelezwa na Serikali.

Prof. Mkumbo alisema hayo katika ziara yake ya kikazi aliyoifanya mkoani Mtwara, alipokuwa akitembelea mamlaka hiyo kwa nia ya kujua utendaji kazi wake na mipango ya utekelezaji wa miradi yake.

“MTUWASA imeshika nafasi ya 8 kati ya mamlaka 25 nchini mwaka huu kulingana na ripoti ya EWURA, ni moja ya mamlaka zinazofanya vizuri. Hivyo, hamna budi kutoka asilimia 60 ya huduma mnayotoa sasa na kufikisha asilimia 100, ili kuendana na mahitaji ya wananchi pamoja na viwanda vikubwa vilivyopo mjini hapa”, alisema Katibu Mkuu.

Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa ili kuendana na Sera ya Viwanda huduma ya maji haina budi kuwa ya uhakika na endelevu, na MTUWASA inabidi wahakikishe Serikali inafanikiwa kufikia lengo hilo kama watoa huduma wa maji.

Aidha, aliwaasa wananchi wa Mtwara kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji, kwani pamoja na juhudi za Serikali za kuwekeza katika miradi mikubwa ya maji, itakuwa ngumu kufanikisha lengo la kutoa huduma ya uhakika na endelevu ya majisafi na salama kama vyanzo vya maji havitatunzwa na kuwa endelevu.

Naye Mkuregenzi Mtendaji wa Mamlaka ya ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA), Inj. Mashaka Sitta alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha mamlaka hiyo inakuwa bora nchini ndani ya miaka miwili; baadhi ya mipango yao ikiwa ni kutunza vyanzo vya maji, kuongeza mitandao ya miundombinu ya maji, kuongeza uzalishaji na wateja ili kufikia lengo hilo.


Katika ziara hiyo Katibu Mkuu alitembelea pia Ofisi za Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya Kusini na kukutana na baadhi ya watendaji wake na kuzungumza nao kuhusu usimamizi na maendeleo ya rasilimali za maji katika bonde hilo na kukamilisha ziara yake ya siku mbili katika mikoa ya Lindi na Mtwara

Comments