Wednesday, June 14, 2017

SERIKALI YAIONGEZEA BAJETI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA NCHINI.


Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imeiongezea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini kiasi cha shilingi bilioni 2.6 katika Bajeti yake ya mwaka 2017/2018 kwa kutambua na kuthamini majukumu yake katika Taifa.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango (MB),Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maaluum (CCM), Mhe. Mwantumu Dau Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuiwezesha Tume hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mhe. Mwantumu Haji amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikitengewa fedha kidogo sana katika bajeti kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo hali inayosababisha Tume hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2017/18, Serikali imetenga bajeti ya Sh. 6,166,978,000 kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 42.31 ya bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo ilikuwa Sh. 3,557,589,200.

Alisema kuwa viwango vya ukomo wa bajeti kwa mafungu, hutegemea vipaumbele vya Taifa na maoteo ya mapato katika kipindi husika hivyo ongezeko la ukomo wa bajeti ya Tume hiyo kwa mwaka 2017/18 linaonesha dhahiri kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Tume hiyo pamoja na majukumu yake.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani il kuhakikisha mafungu yote ya kibajeti ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora yanaendelea kupata fedha za kutosha ili kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tarehe 01/06/2017 Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua mfumo wa ukusanyaji mapato ya ndani ujulikanao kama ‘Revenue Gateway System’ ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali kuimarisha ukusanyaji mapato yake yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi”, alifafanua Dkt. Kijaji.

No comments: