Waratibu Elimu Kata, Waganga wa Vituo vya Afya Wapewa Elimu ya Uhasibu

Mkuu wa Kitengo cha Tehama na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa akizungumza na waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC (hawapo pichani) kuhusu malengo ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Baadhi ya Waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (hayupo pichani) wakati alipofungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Baadhi ya Waratibu wa Elimu Kata kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (hayupo pichani) wakati alipofungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Sehemu ya Waratibu wa Elimu Kata na Waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (hayupo pichani) wakati alipofungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (aliyeketi katikati) akiwa pamoja na baadhi ya waratibu wa elimu kata kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS). Aliyeketi kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa


Na Mathew Kwembe, Mtwara

Waganga wafawidhi wa vituo vya afya, na Waratibu elimu kata kutoka Halmashauri 93 zilizo katika mikoa 13 nchini inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) nchini wameanza mafunzo ya siku mbili juu ya namna ya kutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Tehama na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma na kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi katika mahesabu ya mapato na matumizi ya halmashauri.

Bwana Wengaa alisema kuwa kuunda kwa mfumo huo kutasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku zinasimamiwa vizuri na taarifa za matumizi yake zinatolewa kwa usahihi tofauti na ilivyokuwa mwanzo.Alisema kuwa FFARS itawapatia watoa huduma mfumo sanifu uliorahisishwa ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao. 

Bwana Wengaa aliongeza kuwa FFARS itaweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo katika kufikia malengo ya utoaji huduma na kuhakikisha yanaendana na sheria za manunuzi na utoaji taarifa. “Taarifa hizi zitasaidia Serikali kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongeza uwazi, na hivyo watoa huduma wa afya kuwa na wajibu kwa jamii wanayoihudumia,” alisema.

Alisema kuwa mafunzo hayo yanafanyika katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ambapo waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya wanashiriki.Aliitaja mikoa hiyo 13 kuwa ni pamoja na Mtwara, Lindi, Dodoma, Iringa, Mbeya, Njombe na Morogoro. Mikoa mingine ni Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Kigoma, na Kagera.

Mafunzo hayo yanafanyika katika ngazi ya halmashauri, ambapo mjini Mtwara mafunzo hayo yaliwahusisha waganga wafawidhi wa vituo vya afya, na Waratibu elimu kata kutoka Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bibi Beatrice Dominick, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mhandisi Sambwe Sijabaje alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma wa vituo vya halmashauri hizo mbili kuwa na mfumo maalum wa kuandaa taarifa za mapato na matumizi, na hivyo kuchangia uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alisema kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa mfumo wa kielektroniki ili kuendana na wakati na mabadiliko ya teknolojia na mfumo wwa kujaza vitabu ulioboreshwa ili kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo umeme na kukosekana kwa huduma ya mtandao wa intaneti kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma.

Hata hivyo baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wameiomba Serikali kuwapatia vitendea kazi kama vile Laptop ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi uliokusudiwa.

Mfumo huo wa FFARS unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwanufaisha Waganga wafawidhi wa vituo vya afya, na Waratibu elimu kata kutoka zaidi ya Vituo vya Afya 550, Zahanati 6800, Hospitali za Wilaya 135, na takribani Shule za Msingi na Sekondari 20,000 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Comments