DC SHINYANGA AWAUMBUA HADHARANI VIONGOZI WA UPINZANI WANAOKWAMISHA MIRADI YA MAENDELEO,AONYA SIASA ZA MAJITAKA
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akinywa maji yaliyokuwa yanadaiwa kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Wananchi wa kijiji hicho wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro
Mmoja wa wananchi hao Shija Luhende akiuponda mradi huo wa maji mbele ya mkuu huyo wa wilaya kuwa maji yake ukiyapikia kwenye ugali au wali chakula kina kuwa cha njano kutokana na kuzidi kwa chumvi na hayafai kwa matumizi ya binadamu
Wananchi wakiwa kwenye mradi wa maji kabla mkuu wa wilaya hajaanza kunywa maji hayo
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akinywa maji yaliyokuwa yanadaiwa kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akinywa maji Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Geofrey Mwangulumbi akinywa maji yaliyodaiwa kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu
Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,Geofrey Mwangulumbi akiinua bakuli baada ya kumaliza kunywa maji
Wananchi wakinywamaji hayo ya mradi wa kisima kirefu ambao walikuwa wameukataa baada ya kurishwa maneno kuwa ni mabaya ukipikia chakula kina kuwa cha njano.
Wananchi wakiendelea kunywa maji
Kila mmoja akataka kunywa maji....
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akiwa ameshikilia sahani yenye wali uliopikwa kwa maji yaliyokuwa yanadaiwa kuwa ukiyatumia kwa chakula,chakula kinabadilika na kuwa na rangi ya njano
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akionesha wali uliopikwa kwa maji ya kisima kirefu cha maji...Wali huo haukubadilika rangi... Picha zote na Marco Maduhu-Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amewataka wananchi wa kijiji cha Mwamagunguli kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga kuacha kuchanganya siasa kwenye masuala maendeleo kwani inakwamisha shughuli za maendeleo na kusababisha kero katika jamii.
Matiro ameyasema hayo jana June 21,2017 baada ya kutatua mgogoro wa mradi wa maji ya kisima kirefu katika kijiji hicho ambapo viongozi wa eneo hilo kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kata na wananchi walikuwa hawatumii maji hayo wakidai kuwa yana chumvi na hata yakitumika kupikia chakula yanakibadilisha na kuwa na rangi ya njano.
Kufuatia utata huo wa mradi huo ambao ujenzi wake ulikamilika tangu Mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 294.6,Mkuu huyo wa wilaya aliamua kufika katika kijiji hicho ili kubaini ukweli wa madai ya wananchi hao.
Baada ya kufika katika kijiji hicho akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo pamoja na viongozi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga walizungumza na wananchi wa eneo hilo ambao walisisitiza kuwa maji hayo hayafai mbele ya mkuu wa wilaya.
Mmoja wa wananchi hao,Shija Luhende aliuponda mradi huo wa maji mbele ya mkuu huyo wa wilaya akidai kuwa maji ya mradi huo wa kisima kirefu ukiyapikia kwenye ugali au wali chakula kinakuwa cha njano kutokana na kuzidi kwa chumvi hivyo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya maji katika kijiji hicho Grace Jackson alisema mradi huo wa maji wameshindwa kuuendesha kutokana na kupata hasara kwani kila wanaponunua umeme wa Shilingi 100,000/= kisha kusukuma maji kwenye tanki,wanapouza maji hayo kwa wananchi wamekuwa wakiishia kupata shilingi 3,000/= tu huku maji nayo yakikauka kwenye tanki bila ya kujua yameishaje na hivyo kuona mradi huo hauna faida zaidi ya kupata hasara.
Kufuatia hali hiyo,ili kumaliza utata,mkuu wa wilaya aliagiza maji kutoka kwenye kisima yajazwe kwenye tanki na kusukumwa ili serikali ijiridhishe kama kweli maji hayo yana chumvi nyingi.
Mkuu huyo wa wilaya aliamua kuyanywa maji hayo katika mkutano wa hadhara na kudhibitisha kuwa ni mazuri tena yanafaa kwa matumizi ya binadamu huku viongozi waliokuwa katika mkutano huo pamoja na wananchi wakinywa maji hayo huku wakishangilia kuwa ni maji mazuri hayana chumvi.
Matiro hakuishia kunywa maji tu,pia aliagiza chakula kipikwe jirani na nyumba iliyopo karibu na mkutano huo wa hadhara kisha kiletwe mbele ya wananchi ili kuona kama kimebadilika na kuwa na rangi ya njano.
Chakula kilichopikwa ni wali ambao haukubadilika rangi hali iliyowafanya wananchi waanze minong’ono ya hapa na pale wakidai kuwa walichezewa akili zao kwa kudanganywa na viongozi wao kuanzia ngazi ya kitongoji waliowaaminisha kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.
Baada ya kunywa maji hayo na kuona wali haujabadilika rangi wananchi hao,walianza kutoboa siri kuwa mradi huo uliingizwa siasa ndani yake kutoka kwa viongozi wao kutoka vyama vya upinzani (Chadema) ili serikali ionekane imeanzisha mradi mbovu.
Mmoja wa wananchi hao,Joyce Mugoswa alitoboa siri kuwa maji hayo walikuwa hawajawahi kuyatumia zaidi ya kuambiwa tu kuwa ni mabaya na yana chumvi nyingi na yakipikiwa chakula chote kina kuwa cha njano na hivyo kulazimika kwenda kufuata huduma hiyo ya maji umbali mrefu katika hospitali ya Kolandoto.
"Ukweli mkuu wa wilaya, mradi huu wa maji ulitawaliwa na siasa ,tulikuwa tukiambiwa maji ni mabaya tusichote, tutakufa na hivyo kuingiwa na hofu ,kumbe tunaacha maji mazuri kabisa" ,alisema Magoswa.
Aidha baada ya wananchi kujiridhisha kuwa maji hayo ni salama waliukubali mradi huo wa maji,huku baadhi ya wafuasi wa Chama Cha Maendeleo (Chadema) waliokuwa eneo la mkutano wakianza kuondoka mmoja baada ya mwingine baada ya kuumbuliwa hadharini.
Mkuu huyo wa wilaya alionya siasa kwenye masuala ya maendeleo na kutoa onyo kwa atayeendekeza siasa za maji taka na kukwamisha miradi ya maendeleo kutonufaisha wananchi, atakula naye sahani moja kwa sababu huyo ni mhujumu uchumi .
"Nilichobaini hapa ni kwamba kuna watu wanaleta siasa kwenye masuala ya maendeleo,kamwe hatutakubali kuona watu wanakwamisha shughuli za maendeleo,hebu fikiria akina mama walikuwa wanatumia muda mrefu kufuata huduma ya maji wakati maji yapo hapa tena hayana tatizo lolote,siasa za majitaka zilishapitwa na wakati,huu muda wa kazi tuwaletee maendeleo wananchi", alieleza Matiro.
Matiro aliukabidhi mradi huo chini ya uongozi wa sungusungu ndani ya wiki moja wakishirikiana na wataalam wa manispaa ya Shinyanga ili kuona kama hizo hasara za kuendesha mradi zitajitokeza tena.
Comments