WAZIRI MKUU AONGOZA MAZISHI YA DIWANI WAKE

Waziri  Mkuu Kassim  Majaliwa  na Mbunge wa Ruangwa,  akiweka mchanga  kwenye kaburi la aliyekuwa  Diwani wa  CCM Kata ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw.  Daniel Petro  Mtawa ambaye amefariki tarehe   May 7,2017 na kuzikwa  kijijini  kwake  Nandagala  Wilaya ya Ruangwa  Mkoani  Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
 Waziri Mkuu Kassim  Majaliwa  akitoa salamu za Pole  Katika  Msiba kwa  aliyekuwa Diwani wa  CCM Kata ya Mnacho ,Kijij cha Nandagala , Bw.  Daniel Petro  Mtawa aliyefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa  kijijini  kwake  Nandagala  Wilaya ya Ruangwa  Mkoani  Lindi May 8 ,2017. (PICHA NA OWM)
Waziri  Mkuu  Kassim  Majaliwa  akiwa ameongozana na  Viongozi  wa Mkoa  wa  Lindi na Mtwara   pamoja na wananchi kuelekea makaburini kwa ajili  ya  mazishi ya aliyekuwa Diwani wa  CCM Kata ya Mnacho, Kijiji cha Nandagala , Bw.  Daniel Petro  Mtawa aliyefariki tarehe May 7,2017 na kuzikwa  kijijini  kwake  Nandagala  Wilaya ya Ruangwa  Mkoani  Lindi May 8,2017. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Halima Dendego na wa pili kulia, ni Mkuu  wa Mkoa  wa Lindi,  Bw.  Godfrey  Zambi. Kushoto  ni Kaimu   Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa , Bi. Rukia Mhango. (PICHA NA OWM)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameongoza mamia ya wakazi wa kata ya Mnacho, wilayani Ruangwa kwenye mazishi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Bw. Daniel Mtawa ambaye alifariki dunia Mei 7, 2017. 

Akizungumza na waombolezaji katika ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye kijiji cha Nandagala, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi jana (Jumatatu, Mei 8, 2017), Waziri Mkuu alisema msiba uliowapata wana-Mnacho ni mkubwa, na akatumia fursa hiyo kuwapa pole wanafamilia na wanakijiji wenzake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ruangwa, anatoka katika kijiji cha Nandagala, kwenye kata hiyohiyo ya Mnacho.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. “Mheshimiwa Rais ametoa salamu za pole kwa mke wa marehemu, familia na wana-Ruangwa wote. Pia Mheshimiwa Makamu wa Rais, anawapa pole wana-Ruangwa wote kwa msiba huu mzito,” aliongeza.

“Ndugu yetu Mtawa amemaliza safari yake na ametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumuombea marehemu Mtawa, kila mtu kwa imani yake. Ninatoa pole kwa familia, kwa Mwenyekiti wa Halmashauri na madiwani wenzangu wote,” alisema.

Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ruangwa, Bw. Rashid Nakumbya, alisema Bw. Mtawa alikuwa diwani wa kata hiyo tangu mwaka 2015 lakini alianza kupata tatizo la shinikizo la damu Desemba mwaka jana. “Alilazwa katika hospitali ya Nyangao kwa mwezi mmoja, na baadaye akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alilazwa kwa miezi miwili kabla ya kupata nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani kuendelea na dawa,” alisema.

Marehemu Mtawa ameacha mjane, watoto saba (wa kiume watano na wa kike wawili) na wajukuu wanane.

Kwa upande wake, Mwinjilisti Sebastian Francis wa Kanisa la Anglikana Ruangwa alisema mshahara wa dhambi ni mauti na akawataka waombolezaji wote kila mmoja kwa imani yake wajiepushe na anasa za dunia ili waweze kuurithi ufalme wa mbinguni.

“Baada ya kifo yapo maisha na Bw. Daniel Mtawa amemaliza safari yake, lakini je mimi na wewe tumejiandaa vipi kufika mwisho wa safari yetu? Ndugu zangu, maisha ya starehe na anasa yasitufanye tuukose ufalme wa Mbinguni,” alisema.

Akitoa mfano kutoka kitabu cha Luka (16:19-31) wa Lazaro maskini ambaye alikuwa akiomba chakula lakini hapewi hadi kutamani makombo kutoka kwa tajiri, Mwinjilisti Francis alisema wanadamu tunapaswa kubadilika na kujaliana.

“Huu mfano unaonyesha kuwa hakuna aliyemjali wala hakuna aliyemhudumia yule maskini. Tunafundishwa kuwa watu wa kuhurumiana na kujaliana bila kujali dini, rangi au kabila la mtu,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alirejea Dodoma jana usiku kuendelea na ratiba za vikao vya Bunge.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMANNE, MEI 9, 2017.

Comments