WAZIRI wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kulia akipata maelekezo juu ya nchi zenye ugonjwa wa homa ya manjano barani Afrika na Duniani kutoka kwa Afisa Habari Msaidizi Wa Wizara ya Afya Bw. Ally Daud kushoto mara baada ya kupata chanjo ya homa ya manjano katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma.
Msemaji Mkuu wa Serikali na ambaye ni Mkurugenzi Idara ya Habari Dkt Hassan Abbas wa kwanza kulia akipokea cheti cha homa ya manjano kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Afya Mazingira Dkt. Khalid Massa wa kwanza kulia mara baada ya kupata chanjo hiyo katika viwnja vya Bunge mjini Dodoma katikati ni Afisa Afya Remidius Kakulu.
NA Ally Daud –WAMJW Dodoma.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amewasihi wanamichezo wa Tanzania wapate chanjo ya homa ya manjano kabla ya kusafiri ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano wanapokwenda nchi ambazo zina maambukizi ya ugonjwa huo.
Akizungumza hayo mara baada ya kupata chanjo hiyo katika viwanja vya bunge mjini Dodoma Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wanamichezo wanastahili kupata chanjo hiyo ili wasipate ugonjwa pindi wanapotembelea nchi zenye ugonjwa huo.
“Nawaomba wanamichezo na watanzania kwa ujumla wapate chanjo hii ili kusudi wajilinde kutokupata ugonjwa huu kwani tumezungukwa na nchi wanachama ambao wana ugonjwa wa homa ya manjano” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wanamichezo wanastahili kupata chanjo hiyo kwani huwa wanasafiri mara kwa mara kuwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbas Amesema kuwa ugonjwa wa homa ya manjano una madhara hivyo ni vyema kwa wafanyakazi,wafanyabiashara pamoja na wanafunzi wanaosafiri nje ya nchi hususani nchi zenye ugonjwa huo ni vyema wakajitokeza kupata chanjo.
Comments