WAZIRI LUKUVI AMTUMBUA AFISA MIPANGO MIJI LINDI



 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akimsimamisha kazi Ndugu Castory Manase Nkuli Afisa Mipango Miji wa Lindi kuhusu tuhuma za kumilikisha ardhi kinyume cha sheria.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (kushoto) wakihakiki nyaraka na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi (kulia) katika ziara ya Mhe. Lukuvi mkoani Lindi.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi, watendaji na viongozi wa Mkoa wa Lindi wakiwa katika mkutano wakati wa ziara ya Mhe. Lukuvi mkoani Lindi.
 Kaimu Mkurugenzi wa Mipango Miji na Vijiji Bi. Imaculate Senje akizungumza kuhusu utaratibu za upangaji miji  na umilikishaji ardhi katika ziara ya Mhe. Lukuvi mkoani Lindi.
 Ndugu Castory Manase Nkuli Afisa Mipango Miji wa Lindi akijieleza kuhusu tuhuma zinazomkabili mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi katika ziara ya Mhe. Lukuvi mkoani Lindi.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akikagua mafaili katika masijala ya ardhi mkoani Lindi ambapo alibaini mapungufu ya kutokuwa na usahihi wa uwekaji kumbukumbu za ardhi.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi wakikagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi mkoani Lindi
Ndugu Gibson Mwaigomole Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Lindi
Na. Hassan Mabuye & Muhammad Salim.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameamuru kusimamishwa kazi Afisa Mipango Miji wa Lindi Ndugu Castory Manase Nkuli baada ya kunyang`anya ardhi ya vijiji vya Ruvu na Mchinga hekari 4000 na kumilikisha kampuni ya Azimio Housing Estate kinyume cha sheria ya Ardhi.
Mhe. Lukuvi aligundua hayo baada ya kuona utaratibu wa umilikishaji wa ardhi haukufuatwa  na badala yake kuonekana kuwa na mianya ya rushwa kwa kuwa ardhi hiyo imehamishwa kutoka ardhi ya kijiji hadi kumilikishwa kwa kampuni ya Azimio ambapo kisheria ilitakiwa hati ya eneo hilo itoke kwa idhini ya Rais.
Aidha, Afisa Mipango Miji huyo aligundulika kuwa na kosa la kughushi kwa kujifanya ni Afisa ardhi baada ya kuandika barua na kuisaini kwa niaba ya Afisa ardhi wakati yeye ni Afisa Mipango Miji ili kuimilikisha kampuni ya Azimio Housing Estate ambalo pia ni kosa kisheria.
Akithibitisha makosa hayo Kaimu Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji kutoka Wizara ya Ardhi Bi Immaculate Senje amesema kwamba utaratibu wa umilikishaji wa ardhi hiyo haukufuatwa ambapo kisheria ilitakiwa hati ya eneo hilo itoke kwa idhini ya Rais na baada ya Tangazo la Serikali na kuridhiwa na wana kijiji. 
 “Kama nyie hamna uwezo wa kumfukuza kazi basi mie namsimamisha kazi kuanzia leo hafai kuwa mtumishi wa serkali” alisema Mhe. Lukuvi na kuagiza eneo hilo lirudi na kuwa mali ya serikali “ Sasa hiyo ardhi lazima irudi itakua mali ya serikali kuanzia leo” .
katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi ametembelea ofisi za ardhi Lindi na kufanya ukaguzi katika Masijala za ardhi na kuangalia mfumo wa ukusanyaji kodi ya pango la ardhi, kisha kuwaagiza watendaji wa ardhi mkoani hapo kuhakikisha wanatoa hati kwa wakati na kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa kila mmiliki wa ardhi ili kuongeza pato la serikali.
Pia alitembelea ofisi za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani hapo na kupokea taarifa kutoka kwa Meneja wa shirika hilo mkoani Lindi Ndugu Gibson Mwaigomole. Katika taarifa hiyo Mhe. Lukuvi amelishauri Shirika la Nyumba la Taifa kufanya uwekezaji mkoani Lindi kwa kujenga ofisi za kisasa pamoja na Nyumba zenye gharama nafuu.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Godfrey Zambi akiwa pamoja na waziri Lukuvi na watendaji wa mkoa ameeleza kuwa sekta ya ardhi mkoani hapo inachangamoto nyingi lakini ofisi yake inaendelea kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha changamoto hizo zinapungua au kuzimaliza kabisa kwa maslahi ya watu wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Comments