JPM AWATAKA WAKANDARASI NCHINI KUJITATHMINI

   Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi nchini kujitathmini, kurekebisha makosa yao pamoja na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali badala ya kuilalamikia kuwa haiwasaidii.


Rais Magufuli ameyabainisha hayo wakati akiongea na wafanyabiashara wa sekta binafsi katika mkutano wa 10 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.


Rais Magufuli amesema kuwa tenda mbalimbali za ujenzi wa miundombinu zimekuwa zikitolewa na Serikali mara kwa mara lakini wakandarasi nchini wamekuwa hawazitumii fursa hizo na matokeo yake zinatolewa kwa wakandarasi kutoka nchi zingine.


“Serikali inatangaza tenda nyingi za ujenzi wa miundombinu na kwa kiasi kikubwa huwa inawalenga wakandarasi wa ndani kuliko wanaotoka nje lakini wakandarasi wetu wamekuwa hawazitumii fursa hizo, Serikali itachoka kuwabeba hivyo wakae wajitathmini,” alisema Rais Magufuli.


Ameongeza kuwa wakandarasi wanatakiwa kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili waweze kupata tenda zinazotolewa na Serikali kwa urahisi pia amewataka wawe wazalendo katika upangaji wa bei za kazi zao.


Akitoa mfano wa kukosa uzalendo, Rais Magufuli amesema kuwa wakandarasi wa hapa nchini walipoombwa kutoa bei za ujenzi wa mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walitaja kiasi cha shilingi kati ya bilioni 150 na 200 wakati Wakala wa Majengo (TBA) waliyajenga kwa bilioni kumi tu.


Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wafanyabiashara wa sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na kuwahakikishia kuwa Serikali iko pamoja nao katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.


Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ametoa siku moja kwa taasisi zinazohusika na huduma za bandari zikiwemo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kuanza kutoa huduma zao kwa saa 24.


“Tumeamua kufanya hivyo ili kurahisisha huduma kwa wafanyabiashara kwani wamekua wakipata shida kwa kutumia muda mrefu kupata huduma katika bandari yetu, nafikiri njia hiyo itachochea wafanyabiashara kuwekeza zaidi”, alisema Mhe. Majaliwa


Ametoa rai kwa wafanyabiashara wa sekta binafsi kuwekeza kwenye kilimo kwani maendeleo ya ujenzi wa viwanda unategemea malighafi zinazotokana na kilimo.


Aidha Majaliwa alisema Serikali imekusudia kupanua wigo katika sekta ya kilimo kwa kuleta zana bora za kilimo, kuendelea kupunguza kodi katika mazao pamoja kuiwezesha Benki ya Kilimo kuendelea kutoa mikopo kwa wingi.


Nae, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Dkt. Reginald Mengi ameipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi mbalimbali walizojiwekea zikiwezo za elimu bure, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa ndege pamoja na kukaa na wananchi na wadau mbalimbali kusikiliza na kutatua changamoto zao.


“Ushiriki wa wadau kwenye kikao hiki ni muendelezo chanya wa mahusiano mazuri kati ya Serikali na sekta binafsi, ninaamini majadiliano haya yatatatua changamoto za wafanyabiashara wa sekta binafsi”,alisema Dkt. Mengi.

Comments