Tuesday, June 29, 2010

Marubani wa JWTZ wafa ajalini



WANAJESHI wawili ambao ni marubani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kambi ya Ngerengere mkoani hapa, wamekufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kuligonga gari la watalii na kupinduka.Ndege hiyo ya Jeshi ambayo inatumika katika mafunzo ya kijeshi, jana ilitua barabarani na kusababisha ajali iliyoua marubani wawili wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) baada ya kugongana na lori lililokuwa limebeba watalii.

Ndege hiyo ndogo yenye namba F59119 iligongana na gari hilo eneo maarufu kwa jina la Zimbabwe lililo Kijiji cha Manga, Kata ya Mkata wilayani Handeni.

Baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo ya nadra sana kutokea walieleza kuwa waliiona ndege hiyo ikishuka kabla ya kutua katikati ya barabara na baadaye kujaribu kuruka tena, kitu kinachoonyesha kuwa rubani alikuwa katika harakati za kuinusuru.

Walisema, hata hivyo, ndege hiyo ilishindwa kuruka juu na kuserereka barabarani.
Walisema wakati ikiyumba, ndege hiyo nusura iligonge basi la kampuni ya Simba Mtoto lililokuwa likitokea jijini Tanga kuelekea Dodoma.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Tanga, Jafari Mohammedi ambaye alikuwa kwenye eneo la tukio hilo, aliwataja waliokufa kuwa ni rubani wa ndege hiyo Meja Kathbet Leguna (41) na mwanafunzi wake Luteni Andrew Yohana Kijangwa (31).

Mmoja wa wafanyakazi wa gari hiyo iliyogongana na ndege hiyo Solomon Talalai alisema ndani walikuwepo watu 24 ambao 19 kati yao ni raia kutoka Uholanzi, wanne kutoka Kenya na mmoja Mtanzania. Imeandikwa na Hussein Semdoe na Burhani Yakub, Handeni:SOURCE:MWANANCHI

No comments: