WAGOMBEA wanane kutoka chama cha mapinduzi CCM leo wamechukua fomu za kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar baada ya rais aliyepo madarakani Amani Abeid Karume kumaliza vipindi vyake viwili vya uongozi kwa mujibu wa katiba.
Takriban wagombea wote wanane wanaotaka kuwania kinyanganyiro hicho wamezungumzia suala la kudumisha amani na kuendeleza maridhiano yaliofikiwa na Rais wa Zanzibar Amani Karume na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad. iwapo watapata ridhaa ya wananchi ya kuiongoza Zanzibar.
Wagombea waliochukua fomu leo ni Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha ambaye alichukua fomu saa 3: 00 asubuhi na kuzungumza na waandishi katika Hoteli ya Bwawani. Ali Karume alichukua fomu saa nne asubuhi, Alli Juma Shamhuna alichukua fomu saa tano, Bakari Mshindo saa sita mchana, Dk Billal akachukua saa nane, Dk Shein saa tisa na Mohammed Aboud saa 10 jioni.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu, Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud alisema Zanzibar hivi sasa iko kwenye mazingira mazuri zaidi kuliko nyakati nyingine zozote katika historia yake.
Makamu wa Rais Dk Ali Mohamed Shein aliahidi kuwa atahakikisha Wanzanzibari wanaishi kwa amani na kuendeleza utamaduni wao wa kuvumiliana na kusaidiana.
Akizungumza katika hilo Balozi wa Italia Ali Karume alisema pamoja na kuwa anaunga mkono maridhiano, lakini suala la kura ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ya ndio au hapana hawezi kutaja msimamo wake kwa kuwa kura ya maoni itategemea wakati husika.
Waziri Kiongozi Mstaafu Dk Mohammed Gharib Bilal alisema endapo Wazanzibari watampa ridhaa ya kuongoza ataendesha nchi kwa misingi ya utawala wa sheria huku akisisitiza suala la nidhamu katika utawala wake.
Kamishna wa Elimu na Utamaduni, Hamad Bakari Mshindo alisema kwamba Zanzibar inahitaji mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali kwa ajili ya kuleta maendeleo ikiwemo elimu. Habari ya Salma Said na Picha za Martin Kabemba wa Zanzibar. SOURCE: MWANANCHI
Comments