Sunday, June 06, 2010

Bendera ya Taifa



HUYU jamaa sijui ni kwamba anaipenda nchi yetu au anazuga, lakini habari ndiyo hii raia wa Australia, Jock Biduull amekuwa akiwashangaza mamia ya wakazi wa Arusha kutokana na kuamu kufunga bendera ya Taifa katika gari lake na kuranda nalo mitaani kwa takriban siku tatu sasa.

Raia huyo ambaye yupo nchini akifanya kazi za kujitolea katika shule ya St Jude iliyopo wilayani Arumeru mkoani hapa, ametundika bendera ya Taifa mbele ya gari lake na kuranda nalo mitaali bila hofu.

Hata hivyo, wakati raia wa kawaida wamekuwa wakiona kitendo hicho ni ukiukwaji wa katiba ya nchi hasa kuhusiana na hadhi ya Bendera ya Taifa, lakini hata hivyo hakuna chombo chochote za usalama ambacho kimemkataza.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika eneo la Arusha Hoteli mjini hapa juzi, Biduull alisema ameamua kufunga bendera ya Taifa la Tanzania mbele ya gari lake kutokana na kuipenda nchi hii.

"Mimi sijuwi kama ni kosa ila tangu nimekuja Tanzania nimeipenda sana na nimeona nifunge kwenye gari bendera ya nchi hii,"alisema Biduull.

Mkuu wa kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) mkoani Arusha, Shillinde Ngalula akitoa maoni yake kisheria kuhusiano na kuweka kwenye gari bendera ya Taifa alisema ni makosa mtu asiyeruhusiwa kuiweka.

"Kama ni kweli huyo mzungu anatembea na bendera ya Taifa kwenye gari atakuwa amekiuka sheria ya Nembo za Taifa hivyo ni makosa kwani pia anaweza kusababisha kutisha watu bila sababu za msingi,"alisema Ngalula.

Hata hivyo hakuna afisa wa polisi ambaye alikuwa tayari kuzungumzia ni kwa nini Rais huyo wa Autralia ameshindwa kukamatwa wala kuhojiwa kutokana na kuweka bendera ya Taifa kwenye gari lake na kutamba nayo mitaani. Habari na picha ni za Mussa Juma wa Arusha: SOURCE MWANANCHI.

No comments: