MHAKIKI Kurasa wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, Sunday Citizen na Mwanaspoti, Adam Mwakibinga amefariki dunia baada ya kuugua.
Taarifa zilizotolewa jana na ndugu zake zilieleza kwamba Adam alifariki saa 10 :00 jioni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi kwa muda.
Ndugu hao walisema kuwa mipango ya mazishi ya marehemu Mwakibinga inafanyika jijini Dar es Salaam na Mbeya na taarifa zaidi kuhusiana na mahala yatakapofanyika mazishi zitatolewa leo.
Marehemu Mwakibinga alizaliwa miaka 46 iliyopita mjini Dodoma na alianza elimu yake ya msingi katika shule ya Msingi mwaka 1974 na akahitimu katika shule ya Msingi Mwenge mkoani Tabora.
Baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kazima iliyopo mjini Tabora ambako alihitimu kidato cha nne mwaka 1985.
Mwaka 1986 alijiunga na kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Mkwawa na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1988 akiwa amefanya vizuri katika masomo yake.
Mara baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 1988, Mwakibinga alijiunga na Kozi za uandishi wa habari ngazi ya cheti. Alijiunga na Kampuni ya Mwananchi Communications Julai 10, 2006.
Katika uhai wake marehemu Mwakibinga amewahi kufanya kazi mbalimbali ambapo mwaka 1988 hadi 1995 alifanya kazi ya ukarani wa mapato wa Mamlaka ya Maji Dodoma. Mwaka 1995 alifanya kazi ya usanifu Gazeti la Dar Leo hadi mwaka 2005. Mwaka 2005 hadi 2006 alikuwa Mwakilishi wa Kampuni ya Busines Times Ltd wilayani Rungwe. Marehemu Mwakibinga ambaye hadi anafariki ameacha watoto wawili. Mungu ailaze mahala pema peponi Ameen!
Comments