Friday, December 25, 2009

Yanga washerehekea Xmass kwa bao 2-1




MSHAMBULIAJI Shamte Ally aliyeingia akitokea benchi aliibuka shujaa kwa kufunga bao dakika ya 118 na kuipa Yanga ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Shamte aliyeingia dakika 95 akichukua nafasi ya Abdil Kassimu 'Babi' alipokea pasi nzuri kutoka kwa Ngasa akiwa nje ya eneo la penalti alipiga shuti lilomshinda kipa Juma Kaseja na kutinga wavuni.

Katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote ulishudia dakika tisini zinamalizika kwa timu hizo kwenda sare ya bao 1-1 na kulazisha mchezo huo kuongezwa dakika 30.

Mshambuliaji Jerry Tegete alifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 60 akipokea pasi ya Abdil Babi na kupitisha mpira juu ya kipa Juma Kaseja.

Hillay alifunga mabao la kusawazisha kwa Simba kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Bakari Mohamed kumwangusha kwenye eneo la hatari mshambuliaji Emmanuel Okwi dakika ya 79.

Katika dakika ya 110, Simba ilipata pigo kubwa kwa kutolewa kwa kiungo wake Haruna Moshi Boban aliyepewa kadi nyekundu na mwamuzi Denis Batte kutoka Uganda kwa kitendo cha kutumia maneno machafu kwa mwamuzi msaidizi John Kanyenye.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga itacheza fainali Jumapili dhidi ya Sofapaka, wakati Simba watawania mshindi wa tatu dhidi ya Tusker kesho.

Mwanzoni wa kipindi cha pili timu zote zilirudi kwa kasi ya kutafuta mabao ya mapema lakini hali ya kosa kosa iliendelea vile vile hadi pale Tegete alipofunga bao lake la sita kwenye michuano hiyo.

Yanga iliwatoa kipa Mghana Yaw Berko aliyeumia baada ya kugongana na Mgosi na kumwingiza Obren Cuckovic, pia walimtoa Kigi Makasi kuingia Godfrey Bonny. Huku Simba wakimpumzisha Mgosi na kumwingiza Mike Baraza mchezaji wa zamani wa Yanga.

Muda mfupi baada ya kuingia Baraza alipiga shuti lilopanguliwa kwa ufundi mkubwa na kipa Cuckovic dakika 77.

Kiungo Abdil Kassimu alipiga shuti akiwa katikati ya uwanja, lakini hakulenga goli dakika ya 48, naye Mgosi alikosa nafasi ya wazi baada ya kupewa krosi safi na Kanoni, lakini shuti lake likapaa juu akiwa yeye na goli.

Hadi timu hizo zinahenda mapumziko hakuna aliyebahatika kuziona nyavu za mwenzake, licha ya Yanga kutetawala zaidi katika kipindi hicho.

Mchezaji wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo alitolewa nje dakika 36 baada ya kugongana na Nadir na nafasi yake kuchululiwa na Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Kinara wa ufungaji katika michuano hii alipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 33 aliposhindwa kumalizia pasi aliyopewa na Nurdin Bakari akiwa yeye na goli.

Simba walirudi mchezoni na kufanya shambulizi la kushitukiza katika dakika 26 pale mabeki wa Yanga walipozani wametegea mtego wa kuotea, lakini Nadir Canavaro alikuwa makini kuokoa hatari hiyo. Imeandikwa na
Sosthenes Nyoni, Vicky Kimaro

1 comment:

Anonymous said...

Hasante sana kwa kutuandikia kwa Urefu zaidi...Mdau german