Kigogo wa Richmond aburuzwa kortini



SASA ni dhahiri kwamba, serikali ya Rais Jakaya Kikwete haina mzaha katika kushughulikia tuhuma za ufisadi baada ya kumfikisha mahakamani mfanyabiashara, Naeem Adam Gire kujibu shtaka la kughushi na kutoa taarifa za uongo kuhusu uwezo wa Kampuni ya Richmond.

Tayari serikali imeshawafikisha mahakamani watuhumiwa 21 kwenye sakata la wizi wa jumla ya Sh133 bilioni, mawaziri wawili wa zamani na katibu mkuu wa wizara kwa makosa ya kutumia vibaya ofisi; na jana ilikuwa zamu ya kashfa iliyoitikisa nchi mwaka jana kuhusu utoaji wa zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Richmond.

Kashfa hiyo, iliyoingia hadi ndani ya Bunge la Muungano, ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu baada ya kuhusishwa na sakata hilo. Baadaye mawaziri wawili wa serikali ya awamu ya nne, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha, nao waliachia ngazi.

Jana, Gire alipandishwa kizimbani majira ya saa 9:00 alasiri kujibu tuhuma za kueleza uongo kuwa Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme nchini.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, Wariyalwande Lema, Gire alisomewa mashtaka yake na wakili wa serikali, Boniface Stanslaus ambaye alidai kuwa Machi 13 mwaka 2006 jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alighushi nyaraka akionyesha kwamba, Mohamed Gire, ambaye ni mwenyekiti wa Richmond Development Company LLC ya Texas nchini Marekani, alisaini kumruhusu Naeem Adam Gire kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Comments