Tuesday, June 24, 2025

RAIS SAMIA AWASILI MSUMBIJI KWA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU











MAPUTO – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Maputo, Msumbiji leo tarehe 24 Juni 2025, kwa ajili ya kushiriki katika sherehe kubwa za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Jamhuri ya Msumbiji.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Maputo, Rais Samia alipokelewa kwa heshima zote za kitaifa, kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Rais wa Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, ambaye amemualika kama Mgeni Rasmi katika tukio hilo la kihistoria.

Sherehe hizo zinatarajiwa kufanyika kesho, tarehe 25 Juni 2025, katika Uwanja wa Machava uliopo jijini Maputo, zikihusisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, pamoja na wananchi wa Msumbiji waliojitokeza kuadhimisha mafanikio ya nusu karne tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ureno mwaka 1975.

Ushiriki wa Tanzania katika sherehe hizi ni ishara ya kudumisha uhusiano wa kihistoria na kindugu kati ya Tanzania na Msumbiji, uhusiano ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Samora Machel.

Rais Samia anatarajiwa pia kushiriki katika shughuli nyingine za kidiplomasia ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

No comments:

RAIS SAMIA AWASILI MSUMBIJI KWA SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU

MAPUTO – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili jijini Maputo, Msumbiji leo tarehe 24 Juni 2025, ...