
Dar es Salaam, 18 Juni 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhiwani J. Kikwete, ameongoza ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) uliofanyika jijini Dar es Salaam, na kuelezwa kuwa wa mafanikio makubwa.
Mkutano huo uliambatana na uwasilishaji wa taarifa za kiutendaji za mwaka pamoja na kongamano maalum lililojadili mabadiliko ya sheria za kazi na athari zake kwa waajiri na waajiriwa katika kuongeza tija na ustawi wa mahala pa kazi.
Katika hotuba yake, Waziri Ridhiwani aliipongeza ATE kwa kuendelea kuwa jukwaa imara la kuibua hoja na kutoa mchango wa kitaalamu katika maboresho ya mazingira ya kazi nchini. Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuthamini utatu wa ushirikiano baina ya wadau wakuu wa kazi — Serikali, Waajiri na Wafanyakazi — kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
“Mabadiliko ya sheria za kazi tunayoyasimamia hayalengi kulemaza upande wowote, bali ni kwa lengo la kujenga mazingira bora, yanayolinda haki, lakini pia yanayowezesha ajira endelevu na ufanisi katika sekta binafsi,” alisema Waziri Ridhiwani.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa ATE kwa ushirikiano wao thabiti katika kupitia marekebisho ya sheria na kuhakikisha Tanzania ina sheria rafiki na zinazotekelezeka. Pia aliishukuru jamii ya kimataifa, hususan Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusimamia haki na maslahi ya wafanyakazi.
Waziri Ridhiwani pia aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Cde. Gilbert F. Houngbo, kwa juhudi kubwa zinazofanywa na ATE na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha mazingira ya kazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa maendeleo endelevu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya ajira wakiwemo waajiri, wawakilishi wa mashirika ya wafanyakazi, maafisa wa serikali na washirika wa maendeleo, wote wakijadili njia bora za kuongeza tija, kuboresha sheria, na kukuza ajira nchini.
No comments:
Post a Comment