Sunday, June 15, 2025

RAIS WA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (AfDB), DKT. AKINWUMI ADESINA AMALIZA ZIARA YAKE YA SIKU NNE NCHINI TANZANIA






Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, ambaye anamaliza muda wake wa uongozi, amehitimisha ziara yake rasmi ya kikazi ya siku nne nchini Tanzania. Ziara hiyo ilianza tarehe 12 Juni 2025 na kumalizika tarehe 15 Juni 2025.

Dkt. Adesina aliondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), akisindikizwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Denis Londo.

Ziara hiyo ilifanyika kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa na lengo la kumwezesha Dkt. Adesina kutembelea miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo inatekelezwa kwa ufadhili kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Katika ziara hiyo, Dkt. Adesina pamoja na Rais Samia walitembelea baadhi ya miradi hiyo muhimu jijini Dodoma mnamo tarehe 14 Juni 2025, ikiwemo:

  • Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambao unatarajiwa kuboresha kwa kiwango kikubwa huduma za usafiri wa anga na kuchochea ukuaji wa shughuli za biashara, utalii na uwekezaji katika Ukanda wa Kati;

  • Mradi wa Ujenzi wa Barabara ya Mzunguko ya Jiji la Dodoma, ambao unalenga kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi wa jiji hilo.

Katika kipindi cha uongozi wake, Dkt. Akinwumi Adesina ameiongoza AfDB kwa mafanikio makubwa. Amekuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi ya kitaasisi yaliyoifanya benki hiyo kuwa taasisi imara, yenye mtaji wa kutosha na uwezo mkubwa wa kitaalamu katika kufanikisha miradi ya maendeleo barani Afrika.

Uongozi wake umeweka msukumo mkubwa katika sekta muhimu kama vile miundombinu, kilimo, afya, nishati jadidifu, mabadiliko ya tabianchi, na mifumo ya kifedha. Kupitia AfDB, mataifa mengi yameweza kupata ufadhili wa miradi mikubwa yenye matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.

Kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya bara la Afrika na uongozi wa mfano aliouonesha katika kipindi chake, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetambua juhudi hizo kwa kumtunuku Shahada ya Heshima ya Falsafa katika Sayansi (Doctor of Science - Honoris Causa). Shahada hiyo ilitolewa katika Mahafali ya 55 – Duru ya Kwanza, yaliyofanyika tarehe 13 Juni 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Heshima hiyo ni ishara ya kuthamini kazi kubwa ya Dkt. Adesina katika kuchochea maendeleo endelevu barani Afrika, hususan katika kukuza ushirikiano baina ya taasisi za kifedha na nchi wanachama kama Tanzania.

Kwa ujumla, ziara ya Dkt. Adesina nchini Tanzania imekuwa na mafanikio makubwa na imeonesha uimara wa uhusiano kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Tanzania. Uhusiano huu unaendelea kuwa chachu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.











No comments:

Prof. Mfaransa Aja na Kitabu: Aiambia Dunia Kutalii Tanzania ni Tiba

Na Mwandishi Wetu Paris, Ufaransa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, akiwa nchini Ufaransa jana Julai 8, 2025 amek...