Tuesday, June 17, 2025

WAZIRI RIDHIWANI KIKWETE: FEDHA ZA UNUNUZI WA UMMA ZIWAFIKIE VIJANA, WANAWAKE NA WENYE ULEMAVU



Arusha, Juni 16, 2025 –
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, amehimiza umuhimu wa kuhakikisha makundi maalum nchini yanapata fursa halisi za kiuchumi kupitia zabuni za ununuzi wa umma. Waziri Kikwete ametoa kauli hiyo alipohutubia Kongamano la Ununuzi wa Umma na Ukuaji wa Makampuni ya Wazawa lililoandaliwa na PPRA na kufanyika jijini Arusha.

Kongamano hilo lililolenga kujadili nafasi ya makundi maalum katika uchumi jumuishi kwenye zama za mabadiliko ya teknolojia na kidijitali, limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya manunuzi, maendeleo ya vijana na usawa wa kiuchumi.

Katika hotuba yake, Mhe. Kikwete alisisitiza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamekuwa mahsusi katika kujenga mazingira rafiki kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hasa kwenye maeneo ya fursa za kiuchumi.

"Mabadiliko haya si ya kimfumo tu, bali ni ya kiuwezeshaji – yanalenga kutoa nafasi halisi za kujiendeleza kwa watu wenye mahitaji maalum, kwa njia ya utekelezaji wa sera na sheria zinazowalinda na kuwaimarisha kiuchumi," alisema.

Waziri alieleza kuwa Serikali imeweka msisitizo mkubwa kwenye utekelezaji wa agizo la kisheria la kutenga asilimia 30 ya zabuni zote za ununuzi wa umma kwa makundi maalum, akitaja mambo sita muhimu ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kuwawezesha vijana na watu wenye ulemavu. Hata hivyo, alionya kuwa bado kuna changamoto kubwa ya uelewa mdogo kuhusu uwepo wa fedha hizo, hali inayozuia utekelezaji wake kwa ufanisi.

"Ni wajibu wetu kutoa elimu kwa jamii – madiwani, wakurugenzi wa halmashauri, manispaa na majiji – ili watambue kuwa hizi fedha zipo kwa mujibu wa sheria. Hii itasaidia kuwafikia walengwa kwa haraka na kwa haki," aliongeza.

Waziri pia alikumbusha namna ambavyo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wamekuwa wakichangamkia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, lakini bado kuna nafasi kubwa zaidi kupitia asilimia 30 ya zabuni za serikali.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Kikwete aliipongeza PPRA kwa kuandaa kongamano hilo, akisema limekuja kwa wakati muafaka katika kujenga jamii jumuishi na yenye kuelewa haki zake kiuchumi.

"Ninawashukuru PPRA kwa kazi nzuri na kwa kuona umuhimu wa kuwaelimisha Watanzania kuhusu fursa hizi. Hili ni jukwaa muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wote," alisema.

Kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuhamasisha ushiriki wa wazawa kwenye shughuli za manunuzi ya umma, sambamba na kuwajengea uwezo ili kushindana katika soko la ushindani wa haki.

No comments:

PPAA yatoa rai wazabuni kutumia moduli kuwasilisha rufaa

  Na Mwandishi wetu, Dar Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malal...