Monday, June 16, 2025

WASIRA: UMOJA NA AMANI NDIO MIZIZI YA CCM, TUNU YA TAIFA LETU







Na Mwandishi Wetu

MBOGWE, GEITA – Umoja wa kitaifa, amani na wajibu wa kuwatumikia Watanzania – hayo ndiyo misingi mikuu inayokifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiendelee kuwa imara na cha kuigwa katika bara la Afrika, amesema Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira.

Akizungumza leo Juni 16, 2025, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya siku tatu wilayani Mbogwe, mkoani Geita, Wasira amesisitiza kuwa uhai wa CCM unatokana na mizizi yake iliyojaa historia, utumishi kwa wananchi na maadili ya uongozi wa pamoja.

"CCM si chama cha leo wala kesho tu – ni taasisi ya kihistoria iliyorithi misingi thabiti kutoka TANU na Afro Shirazi Party," alisema Wasira mbele ya viongozi wa CCM wa Wilaya ya Mbogwe pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo viongozi wa dini, wakulima na wafugaji.

Alisema kuwa historia ya CCM si tu kumbukumbu ya miaka, bali ni kielelezo cha dhamira ya kudumu ya kudumisha umoja na ustawi wa Watanzania.

“Watu wengi wanadhani CCM ina miaka 48, lakini TANU ina miaka 75 na Afro Shirazi Party ina miaka 67. CCM ni urithi wa vyama hivyo viwili na ndiyo maana majukumu yake ni ya kudumu. Ndiyo maana tunasema Kidumu Chama Cha Mapinduzi kwa sababu ni kauli ya ukweli, si utani,” alifafanua.

Wasira alibainisha kuwa kazi kuu ya CCM ni kuendeleza misingi ya mshikamano, usawa na utulivu—tunu ambazo zimeifanya Tanzania kuwa tofauti na mataifa mengine mengi ya Afrika.

“Nchi yetu haijajengwa kwa msingi wa udini au ukabila, bali kwa mshikamano. Hii ndiyo silaha ya maendeleo na amani yetu. CCM imepewa jukumu la kulinda tunu hizo kwa niaba ya Watanzania wote,” alisema.

Aliwataka wana CCM na Watanzania kwa ujumla kuendeleza moyo wa umoja na kupokea mawazo mapya kwa namna jumuishi, akisema kuwa jambo lolote likikubaliwa na jamii nzima linakuwa si la mtu mmoja tena, bali tunu ya wote.

Katika ziara hiyo, Wasira anatarajiwa kuendelea na mikutano ya hadhara, vikao na makundi mbalimbali ya jamii ili kuhamasisha mshikamano, kupima uhai wa chama na kufanikisha mazungumzo yenye lengo la kulijenga Taifa kwa misingi ya haki, upendo na maendeleo ya wote.

No comments:

Prof. Mfaransa Aja na Kitabu: Aiambia Dunia Kutalii Tanzania ni Tiba

Na Mwandishi Wetu Paris, Ufaransa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, akiwa nchini Ufaransa jana Julai 8, 2025 amek...