Tuesday, June 17, 2025

NHC KUFANYA MAGEUZI MAKUBWA KARIAKOO: NYUMBA CHAKAVU KUVUNJWA, MAJENGO YA KISASA KUJENGWA























Dar es Salaam, Juni 16, 2025 – Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza rasmi utekelezaji wa mpango mkubwa wa kuibadilisha kabisa sura ya eneo la Kariakoo kwa kulivua gamba la majengo chakavu na kulijengea majengo ya kisasa yanayolingana na mahitaji ya sasa ya makazi, biashara na maendeleo ya miji.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdalah, amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo, Shirika hilo linatarajia kuvunja na kujenga upya majengo yote chakavu ya NHC yaliyopo Kariakoo, na kuyaweka kwenye hadhi mpya ya majengo ya kisasa, ya kuanzia ghorofa 10 kwenda juu.

"Hakutakuwa tena na jengo chakavu la NHC katika Kariakoo ndani ya miaka mitatu. Tayari tumeanza na miradi 16 ambapo majengo ya zamani yamevunjwa na ujenzi wa mapya unaendelea. Kwa ujumla, majengo 64 yataondolewa na kujengwa upya kama sehemu ya mageuzi haya ya kimkakati," alisema Hamad.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, miradi hiyo inatekelezwa kwa mfumo wa ubia baina ya NHC na sekta binafsi, pamoja na ujenzi unaofanywa moja kwa moja na Shirika lenyewe. Hii ni kwa lengo la kutumia vyema rasilimali ardhi, kuongeza mapato ya Shirika na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya ujenzi na makazi.

"Ni muda wa kufanya matumizi bora ya ardhi, hasa katika maeneo ya kibiashara kama Kariakoo. Tunataka kila kipande cha ardhi ya NHC kitumike kwa tija zaidi, na kwa namna inayolipa kiuchumi na kijamii. Majengo haya mapya hayatakuwa tu ya makazi, bali yatachanganya biashara, huduma, ofisi na maeneo ya kijamii," alifafanua.

Mradi huu wa mageuzi ya Kariakoo ni sehemu ya mkakati mpana wa NHC wa kuimarisha uwekezaji wake katika maeneo ya kimkakati (prime areas) kote nchini, hususan mijini, ili kuchangia moja kwa moja katika kubadilisha sura ya miji ya Tanzania kuwa ya kisasa, yenye miundombinu rafiki na inayovutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Hamad alisisitiza kuwa Shirika linaendelea kujiimarisha zaidi katika kusimamia miradi kwa uwazi na weledi, huku likiendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kwa lengo la kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.

"Hili si tu suala la ujenzi wa majengo, ni mageuzi ya fikra kuhusu namna tunavyotumia ardhi, namna tunavyojenga miji yetu na namna tunavyoweka msingi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo," alisema kwa msisitizo.

Kikao hicho na Wahariri ni sehemu ya ziara ya Jukwaa la Wahariri kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na NHC, ikiwa ni pamoja na Kawe 711, GPR Kawe, Samia Housing Scheme na sasa Morocco Square, ambapo wamejionea kwa macho viwango vya juu vya utekelezaji wa miradi ya kisasa ya makazi na biashara nchini.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile, akizungumza mara baada ya ziara ya kutembelea miradi mikubwa minne inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) – Kawe 711, GPR, Samia Housing Scheme Phase II, pamoja na Morocco Square – alieleza kufurahishwa kwake na waandishi wa habari wenzake juu ya hatua kubwa zinazochukuliwa na shirika hilo katika kuanzisha miradi mipya ya ujenzi pamoja na kumalizia miradi iliyokwama kutokana na changamoto mbalimbali za kiutekelezaji.

Bw. Balile alibainisha kuwa, kwa muda mrefu sekta ya nyumba imekumbwa na changamoto za upungufu wa makazi, na jitihada zinazofanywa na NHC hivi sasa ni ushahidi kuwa kuna dhamira ya dhati ya kutatua changamoto hiyo. Alisisitiza kuwa kasi iliyopo sasa ya utekelezaji wa miradi ya makazi inapaswa kuongezwa na kuendelezwa kwa nguvu zaidi ili kuchangia kupunguza pengo kubwa la upungufu wa makazi nchini, ambalo kwa sasa linakadiriwa kufikia nyumba milioni 3.8.

Alitoa rai kwa wadau mbalimbali – wakiwemo sekta binafsi, taasisi za kifedha, na Serikali – kuunga mkono juhudi za NHC ili kufanikisha mpango wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora na salama kwa gharama nafuu. Pia alisisitiza umuhimu wa uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, na matumizi ya vyombo vya habari katika kutoa elimu na taarifa kuhusu miradi hii ili kuongeza uelewa na ushiriki wa jamii.

Akijibu maswali ya wahariri, Hamad alisema Shirika limefanya mabadiliko ya master plan ya mradi wa Kawe 711 ili kuingiza eneo la michezo la kisasa, kufuatia agizo la serikali la kutenga sehemu ya ardhi kwa ajili ya Sports Arena. “Tumejipanga vizuri. Tutakuwa na eneo maalum kwa ajili ya michezo la kisasa, na tuko tayari kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji huu,” alisema Hamad, akiweka wazi kuwa mashauriano ya ubia yataendelea kwa uwazi.

Hamad aligusia moja kwa moja kuhusu gharama za miradi ya nyumba, hasa Kawe, ambapo alisema kusimama kwa mradi kwa miaka nane kumeongeza gharama kwa kiwango kikubwa. “Tulilazimika kufanya re-pricing. Nyumba iliyokuwa inauzwa kwa milioni 80 miaka nane iliyopita, leo gharama zake zimeongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya vifaa na mabadiliko ya kiuchumi. Hii ni changamoto ya kweli kwa walaji, lakini dhamira yetu ni kuhakikisha tunatoa makazi bora kwa bei rafiki kadiri ya uwezo wa soko.”

Kuhusu eneo la kiwanda cha zamani cha Urafiki, Hamad alisema: “Teknolojia ya pale imepitwa na wakati, baadhi ya mashine ni chakavu na hazifai tena. Hata hivyo, tunaangalia uwezekano wa kuweka kiwanda kipya cha kisasa, cha mabati au vifaa vya ujenzi.” Alisisitiza kuwa shirika lina nia ya kuendelea kutumia eneo hilo kwa tija, lakini pia bila kupoteza muda wala mapato.

Mkurugenzi huyo alifichua kuwa sehemu ya milango na vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika miradi ya shirika, tayari huzalishwa na kiwanda cha NHC kilichopo Mpiji. “Hata milango ya miradi ya serikali tunayojenga, sisi wenyewe tumeizalisha. Tunajivunia ubora na tutaendelea kuboresha zaidi,” alieleza kwa fahari.

Hamad pia alizungumzia mpango mkakati wa kuboresha nyumba za zamani, hususan maeneo ya Sinza na jirani. “Tumeanza na matengenezo ya kina: mfumo wa maji safi, maji taka, rangi na mandhari ya jumla. Lakini zaidi ya hayo, tunaanza kampeni ya kubadili fikra za wapangaji.” Alitoa mfano: “Huwezi kupanda na kufuga kuku juu ya ghorofa. Tunataka ustaarabu. Tunataka wapangaji waishi kwa heshima, kwani makazi ni utu.”

Kwa ujumla, kikao hicho kimeonesha dhamira ya NHC kujitathmini na kujipanga upya katika kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, mazingira rafiki na fursa za kijamii na kiuchumi kupitia miradi bunifu. Mkurugenzi Mkuu Hamad Abdallah alimaliza kwa kusema: “Sisi siyo tu tunajenga nyumba – tunajenga maisha.”

No comments:

PPAA yatoa rai wazabuni kutumia moduli kuwasilisha rufaa

  Na Mwandishi wetu, Dar Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imetoa rai kwa wazabuni kutumia Moduli ya kupokea na kushughulikia malal...