Dar es Salaam, Juni 16, 2025 – Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza rasmi utekelezaji wa mpango mkubwa wa kuibadilisha kabisa sura ya eneo la Kariakoo kwa kulivua gamba la majengo chakavu na kulijengea majengo ya kisasa yanayolingana na mahitaji ya sasa ya makazi, biashara na maendeleo ya miji.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na Jukwaa la Wahariri Tanzania, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdalah, amesema kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo, Shirika hilo linatarajia kuvunja na kujenga upya majengo yote chakavu ya NHC yaliyopo Kariakoo, na kuyaweka kwenye hadhi mpya ya majengo ya kisasa, ya kuanzia ghorofa 10 kwenda juu.
“Hakutakuwa tena na jengo chakavu la NHC katika Kariakoo ndani ya miaka mitatu. Tayari tumeanza na miradi 16 ambapo majengo ya zamani yamevunjwa na ujenzi wa mapya unaendelea. Kwa ujumla, majengo 64 yataondolewa na kujengwa upya kama sehemu ya mageuzi haya ya kimkakati,” alisema Hamad.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, miradi hiyo inatekelezwa kwa mfumo wa ubia baina ya NHC na sekta binafsi, pamoja na ujenzi unaofanywa moja kwa moja na Shirika lenyewe. Hii ni kwa lengo la kutumia vyema rasilimali ardhi, kuongeza mapato ya Shirika na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia sekta ya ujenzi na makazi.
“Ni muda wa kufanya matumizi bora ya ardhi, hasa katika maeneo ya kibiashara kama Kariakoo. Tunataka kila kipande cha ardhi ya NHC kitumike kwa tija zaidi, na kwa namna inayolipa kiuchumi na kijamii. Majengo haya mapya hayatakuwa tu ya makazi, bali yatachanganya biashara, huduma, ofisi na maeneo ya kijamii,” alifafanua.
Mradi huu wa mageuzi ya Kariakoo ni sehemu ya mkakati mpana wa NHC wa kuimarisha uwekezaji wake katika maeneo ya kimkakati (prime areas) kote nchini, hususan mijini, ili kuchangia moja kwa moja katika kubadilisha sura ya miji ya Tanzania kuwa ya kisasa, yenye miundombinu rafiki na inayovutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, Hamad alisisitiza kuwa Shirika linaendelea kujiimarisha zaidi katika kusimamia miradi kwa uwazi na weledi, huku likiendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vya habari kwa lengo la kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa uwazi.
“Hili si tu suala la ujenzi wa majengo, ni mageuzi ya fikra kuhusu namna tunavyotumia ardhi, namna tunavyojenga miji yetu na namna tunavyoweka msingi wa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo,” alisema kwa msisitizo.
Kikao hicho na Wahariri ni sehemu ya ziara ya Jukwaa la Wahariri kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na NHC, ikiwa ni pamoja na Kawe 711, GPR Kawe, Samia Housing Scheme na sasa Morocco Square, ambapo wamejionea kwa macho viwango vya juu vya utekelezaji wa miradi ya kisasa ya makazi na biashara nchini.
No comments:
Post a Comment