▪️Rais Samia atajwa kwa kuvutia uwekezaji
▪️Wapongeza mchango wa sekta ya Madini kwenye uchumi wa nchi
▪️Kutoa ruzuku ya euro 60 milioni kuendeleza miundumbino,uongezaji thamani na Utafiti wa kina wa madini
▪️Waziri Mavunde asisitiza juu ya mkakati wa kuongeza thamani madini nchini
Dodoma
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde leo amekutana na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya(EU) kujadiliana juu ya maendeleo ya sekta ya madini nchini na hasa uendelezaji wa madini mkakati.
Ujumbe huo umeongozwa na Mkuu wa Kitengo cha siasa wa Umoja wa Ulaya Bi. Isabelle Mignucci ambaye amepongeza hatua kubwa ya mageuzi ya sekta ya madini yanayofanyika katika kuchangia kukuza uchumi wa Tanzania chini ya uongozi wa Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan.
Jumuiya Ya Ulaya imeonesha utayari wa kuunga mkono jitihada kubwa za kuendeleza sekta ya madini nchini kwa kutenga kiasi cha euro 60 milioni ambayo itaelekezwa katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo ujenzi wa miundombimbu ya barabara kwa maeneo ya uchimbaji,upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika,kuwajengea uwezo watanzania kupitia mafunzo ya ufundi na kufanya utafiti wa kina wa madini katika maeneo mbalimbali chini.
Akizungumza katika mkutano huo,Waziri Mavunde amepongeza hatua ya Umoja wa Ulaya kushirikiana na Tanzania kwenye kukuza na kuendeleza sekta ya madini na kusisitiza kwamba pamoja na eneo la utafiti wa kina ambalo lina umuhimu mkubwa katika kuendeleza sekta ya madini lakini amesisitiza ushirikiano mkubwa zaidi katika uongezaji wa thamani madini nchini ili kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na kuongeza nafasi za ajira zaidi.
“Kipaumbele kikubwa kwa sasa nchini kwetu ni kuona madini yetu yanaongezwa thamani nchini ili tuweze kupata manufaa zaidi.
Hivyo ushirikiano wetu pia lazima uliangalie kwa kipekee hili eneo kwa kuvutia uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani nchini”Alisema Mavunde
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Taaisisi ya Jiolojia na Utafiti wa madini (GST)Dkt. Musa Budeba na Kamishna Msaidizi wa Madini Eng. Terence Ngole
No comments:
Post a Comment