MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam,Albert Chalamila ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilaya ya Ubungo nakutoa maagizo ikiwa ni sehemu ya juhudi za utekelezaji wa miradi ya serikali.
Miradi aliyotembelea ni ujenzi wa Kituo cha Kusukuma maji Kibamba, Kituo cha Afya Mpiji magoe na kuzindua jengo la mama na mtoto pamoja na kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Goba kulangwa.
Chalamila alitoa maagizo hayo jana Aprii 9,2025,wakati wa ziara ya kukagua na kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi wilayani humo na kutoa maagizo kwa viongozi wa halmashauri na wakandarasi kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Amesema miradi hiyo imejengwa kwa kutumia fedha za serikali pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri hivyo ni vyema ikajengwa kwa ubora.
“Naagiza kituo hiki cha kusambaza maji kikamilike haraka ilikiweze kusambaza maji katika jimbo la Ubungo,Segerea,Ukonga na Ilala kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza kama si kuondoa kero ya maji katika maeneo hayo,”amesema Chalamila
Akiwa katika Kituo cha Afya Mpiji Magoe aliagiza fundi alietengeneza viunzi vya milango ya kituo hicho pamoja na sehemu za kutolea maji kutumia fedha zake kuvirudia kwani vimetengenezwa kwa kiwango cha chini na akishindwa kufanya hivyo sheria kali dhidi yake zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupelekwa polisi au magereza ilikurekebisha milango iliyoharibika kutokana na sababu mbalimbali.
“Kituo hiki kinatakiwa kuwa mfano wa utoaji huduma bora pamoja na hili la fundi natoa wito kwa watumishi wa afya kuwa waadilifu, wakarimu, na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma stahiki na kwa wakati,” amesema Chalamila.
Aidha, Chalamila aliagiza kituo hicho kikamilike kwa wakati ilikiweze kuhudumia watu zaidi ya elfu 19000 kutoka maeneo ya Mbezi pamoja na Goba.
Sambamba na hilo Chalamila amemuagiza Mkuu Wilaya hiyo pamoja na Mkurungenzi kuhakikisha cha kituo Polisi cha Tegeta A kinakamilika kwa wakati ilikiweze kusaidia hasa nyakati hizi za kuelekea uchaguzi mkuu.
“Moja ya agizo la rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha serikali za mitaa zinashirikiana na wizara ya mambo ya ndani na sasa hivi tunakabiliwa na uchaguzi mkuu na moja ya silaha ya uchaguzi ni ulinzi hivyo basi tufanye kila linalowezekana kituo hiki kikamilike na askari wawekezaji ilikukabiriana na waarifu pamoja na kulinda amani ya wananchi,”amesema Chalamila
Pia, Chalamila amesema ni vyema shule hiyo mpya ikajengewewa ukuta ili kuitofautisha na shule ya msingi iliyopo eneo hilo ili wanafunzi hao waone fahari ya kusoma katika shule hiyo hata kama wametoka katika shule hiyo ya msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange amesema watayafanyia kazi yaleyote waliyoelekezwa ilikuleta maendeleo na kukuza pato la Taifa.
Hata hivyo ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kibamba utagharimu Sh bilioni 30,Kituo cha Afya mpiji magoe Sh bilioni 615 huku shule ikigharimu fedha kiasi cha Sh bilioni 47 hadi kukamilika
No comments:
Post a Comment