Sunday, April 13, 2025

UBUNIFU NA TEKNOLOJIA: MSINGI WA USIMAMIZI BORA WA MISITU NA NYUKI

 




Na Mwandishi Wetu, Arusha

Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, amewataka Maafisa na Askari wa uhifadhi nchini kuhakikisha wanazingatia mafunzo ya uongozi waliyopata, huku wakiongeza ubunifu na kutumia teknolojia za kisasa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Prof. Silayo aliyasema hayo Aprili 12, 2025, wakati akifunga rasmi mafunzo ya uongozi kwa wahifadhi 481 katika Chuo cha Misitu (Olmotonyi), Jijini Arusha. 

Alisisitiza kuwa elimu waliyoipata inapaswa kuwa chachu ya mabadiliko chanya ya utendaji kazi ili kufanikisha malengo ya taasisi kwa wakati na kwa ufanisi.

“Ni muhimu kila mmoja akasimamia vyema eneo lake la kazi alilokasimiwa. Hii italeta matokeo bora na kusaidia taasisi kufikia malengo yake kwa wakati,” alisema Prof. Silayo.

Aidha, Kamishna huyo alihimiza matumizi ya teknolojia mpya kama matumizi ya drone katika kusimamia maeneo ya hifadhi, akisema teknolojia hiyo itarahisisha utambuzi wa matukio ya uhalifu kwa haraka, hivyo kuongeza ufanisi wa operesheni za uhifadhi.

“Taasisi yetu inatekeleza majukumu mengi muhimu kama upandaji miti, uvunaji wa malighafi, ufugaji nyuki, na utalii wa ikolojia. 

Tunapaswa kuhakikisha jamii inazifahamu shughuli hizi ili kuongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi,” aliongeza.

Aliwahimiza wahifadhi kuondokana na utendaji kazi wa kimazoea na badala yake kuonyesha ubunifu unaoleta matokeo chanya katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki.

Katika kuhitimisha, Prof. Silayo aliwakumbusha wahitimu hao umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria, nidhamu, na ushirikiano kazini, akisema haya ni msingi wa utendaji bora na mafanikio ya Jeshi la Uhifadhi.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi, Dkt. Joseph Makero, aliwapongeza wahitimu kwa nidhamu, ukakamavu na weledi waliouonyesha wakati wote wa mafunzo, akisema sifa hizo ni muhimu katika kutekeleza majukumu ya kitaifa ya uhifadhi.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Utawala wa TFS, Erasto Luoga, aliwasilisha taarifa ya mafunzo hayo na kusema kuwa jumla ya wahifadhi 481 wamehitimu kwa mafanikio makubwa.

No comments:

TANZANIA AND BURKINA FASO IN TALKS TO ESTABLISH CARDIAC FACILITY MODELED AFTER JAKAYA KIKWETE CARDIAC INSTITUTE

  On April 17, 2025, in Ouagadougou, the Executive Director of Muhimbili National Hospital, Prof. Mohamed Janabi @ProfJanabi, along with the...