Monday, April 14, 2025

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWAONGOZA MAWAKILI WA SERIKALI KATIKA MKUTANO MKUU WA MAWAKILI










Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, Mhe. Hamza S. Johari amewaongoza Mawakili wa Serikali kushiriki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali unaofanyika  Jijini, Dodoma tarehe 14 hadi 15 Aprili, 2025.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka Mawakili wa Serikali kuutumia mkutano katika kujadili kwa kina masuala mbalimbali yanayohusu Chama cha Mawakili wa Serikali pamoja na Sekta ya Sheria kwa ujumla.

“Wote tunafahamu lengo la mkutano huu ni kutoa fursa kwa wanachama kujadili mambo mbalimbali yanayohusu chama chetu.”

Katika hatua nyingine, Mhe. Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali kuendelea kutekeleza majukumu yao vizuri ili kuweza kuifikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka  2050, kwa kuzingatia na kuiishi kauli mbiu ya mkutano huo inayosema “Utawala wa Sheria katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali, ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”. 

“Kauli mbiu yetu ya Mwaka huu imejielekeza kwenye Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 na ili tuifikie dira hii tunatakiwa kuwa na proper legal framework na sisi tunataka kuwa facilitator wa kulifikisha taifa huko.”

Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel M. Maneno amewahakikishia Mawakili wa Serikali kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Mawakili wa Serikali wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa ujasiri na ulinzi mkubwa bila kutetereka.

“Tutahakikisha kila Mwanasheria kule aliko anatekeleza  majukumu yake kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na milango ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu iko wazi wakati wowote tutawasikiliza.”

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Ndg. Shaaban Ramadhan Abdalla ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania kwa kuialika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kuja kuhudhuria Mkutano huo huku akikipongeza Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kuendelea kuwasimamia vizuri Mawakili wa Serikali.

Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali umeanza tarehe 14 Aprili, 2025 kwa Mawakili wa Serikali kupokea taarifa mbalimbali zinazohusu chama hicho na Mkutano utaendelea hadi tarehe 15 Aprili, 2025 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Aidha, kupitia mkutano huo Mawakili hao watapata fursa ya kufanya uchaguzi kwa kuwachagua viongozi mbalimbali wa kukiongoza  Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja

No comments:

RAIS SAMIA AKABIDHIWA NAKALA TATU ZA SHERIA ZA TANZANIA ZILIZOFANYIWA UREKEBU – ATOA WITO WA KUZIELEWA NA KUZITUMIA KWA MANUFAA YA TAIFA

Dodoma, 23 Aprili 2025 – Ikulu Chamwino Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amepokea rasmi na...