Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antipas Lissu, amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kufuatia tuhuma za kutoa matamshi ya uchochezi kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Tukio hilo limetokea Aprili 9, 2025, katika mtaa wa Soko Kuu, Wilaya ya Mbinga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chilya, Lissu alikamatwa wakati wa ziara yake ya kisiasa ambapo inadaiwa alitoa kauli zinazoweza kuashiria kuvuruga mchakato wa uchaguzi mkuu ujao.
Jeshi la Polisi limesema kuwa uchunguzi kuhusu tuhuma hizo ulikuwa unaendelea kwa muda kabla ya kuchukuliwa hatua ya kumkamata. Baada ya kukamatwa, Lissu alihamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano zaidi na maafisa wa upelelezi.
Kamanda Marco Chilya ameongeza kuwa uchunguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria ili kubaini kama kuna msingi wa kisheria wa kumfikisha mahakamani.
Jeshi la Polisi limeonya vyama vyote vya siasa na viongozi wao kuwa makini na kauli wanazotoa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Limeeleza kuwa litafuatilia kwa karibu matamshi ya kisiasa yanayotolewa kwenye mikutano, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Aidha, limewataka wanasiasa kujiepusha na lugha ya kukashifu vyombo vya dola au serikali kwa ujumla, kwani kufanya hivyo kunaweza kuchochea uvunjifu wa amani na kuathiri usalama wa taifa. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na sheria.
Viongozi wa kisiasa wamehimizwa kufuata sheria na kutumia njia halali katika kuwasilisha hoja au malalamiko yao. Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linafanya kazi ya kusimamia sheria kwa haki bila upendeleo na kwamba halitavumilia vitendo vya kuchochea machafuko.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda amani, usalama wa raia na mali zao, hasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu. Wamewahakikishia wananchi kuwa usalama wao utaendelea kulindwa kikamilifu
No comments:
Post a Comment