Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST Jijini Arusha
Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Bi. Florida Mapunda akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Kaskazini jijini Arusha
Na Mwandishi wetu, Arusha
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendelea na zoezi la kuwajengea uwezo wazabuni kuhusu matumizi ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo (NeST).
Akifungua mafunzo ya siku mbili (tarehe 10 – 11 Aprili, 2025) kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa Umma kutoka taasisi za Serikali kwa Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika jijini Arusha, Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando amewasihi kujifunza matumizi ya moduli hiyo ili waweze kuitumia kwa ufasaha na kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha.
Bw. Sando amesema kuwa moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki inafaida nyingi kwa wazabuni, taasisi nunuzi na PPAA kwa kuwa inarahisisha zoezi la uwasilishaji na ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma.
“Moduli hii ina faida kadhaa zikiwemo kumsaidia mzabuni kutolazimika kufika katika ofisi za taasisi nunuzi au za PPAA ili kuwasilisha lalamiko au rufaa yake na kupunguza gharama na muda kwa wazabuni kwa kuwa hawatatakiwa kusafiri ili kuweza kuwasilisha malalamiko au rufaa zao,” alisema Bw. Sando
Kadhalika, Bw. Sando ameainisha faida nyingine zinazotokana na matumizi ya moduli kuwa ni kuongeza uwazi katika mchakato wa ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa kwa kuwa mzabuni aliyewasilisha lalamiko au rufaa ataweza kuona hatua mbalimbali za ushughulikiaji wa lalamiko au rufaa yake.
Pamoja na mambo mengine, Bw. Sando amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, PPAA imeweza kushughulikia mashauri 171 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya Ununuzi wa Umma, ambapo katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 36 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika.
“PPAA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa Umma nchini, imeweza kushiriki katika kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 na Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2025,” aliongeza Bw. Sando.
Kwa upande wake Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Huduma za Sheria PPAA, Bi. Florida Mapunda amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wadau wa ununuzi wa umma kuhusu matumizi ya moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST katika Kanda ya Kaskazini.
“Mtakumbuka kwa sasa Sheria ya Ununuzi wa Umma imeweka takwa la ulazima wa ununuzi wa umma kufanyika kwa njia ya Kieletroniki kupitia mfumo wa NeST. Kutokana na takwa hilo, PPAA imejenga moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko katika mfumo wa NeST ili kuwasaidia wadau wa ununuzi kuwasilisha malalamiko na rufaa kieletroniki pia,” alisema Bi. Mapunda.
Bi. Mapunda aliongeza kuwa, moduli imerahisisha zoezi la uwasilishaji wa malalamiko yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma pamoja na kusaidia utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za malalamiko na rufaa ambazo zitakuwa zinawasilishwa katika michakato yote ya ununuzi wa umma.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya usambazaji wa vifaa mbalimbali kutoka Karatu ‘Gratian General Supplies’ Bi. Hilaria Joseph ameipongeza PPAA kwa kuandaa semina hiyo kwani imewasaidia kujua njia ya kuwasilisha malalamiko kwa wakati kupitia kwenye moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki katika mfumo wa NeST.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa Kanda ya Kaskazini yamefanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 10 – 11 Aprili, 2025 yanajumuisha mikioa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Awamu ya kwanza ya mafunzo kikanda yalifanyika Kanda ya Ziwa kwa siku tatu ambapo yalijumuisha washiriki zaidi ya 580 mkoani Mwanza kuanzia tarehe 4 – 6 Februari, 2025 yakijumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Simiyu na Shinyanga.
No comments:
Post a Comment