Wednesday, September 07, 2011

Rais Kikwete akutana na Nizar Khalfan


Mtanzania anayecheza Soka ya kulipwa katika timu ya White Caps ya jijini Vancouver Canada Nizar Khalfan akimkabidhi Rais Dkt.Jakaya Kikwete jezi ya timu yake wakati alipokwenda kumsalimu na kumshukuru ikulu jijini Dar es Salaam jana jioni.(picha na Freddy Maro)

Mchezaji maarufu wa soka wa kimataifa wa Tanzania, Nizar khalfan, ameishukuru Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa misaada mingi ambayo Serikali hiyo imekuwa inatoa kwa wanamichezo, wakiwemo wanasoka na hatua nyingine za Serikali hiyo kuunga mkono jitihada za wanamichezo wa Tanzania.

Aidha, Nizar Khalfan amemshukuru Rais Kikwete kwa jitihada binafsi ambazo hatimaye zimechangia katika mafanikio ya Nizar Khalfan katika soka. Mwanasoka huyo wa Tanzania sasa anacheza soka ya kulipwa katika timu ya Whitecaps ya Canada.

Mwanamichezo huyo alimmwagia sifa Rais Kikwete na Serikali yake wakati alipokutana na kufanya naye mazungumzo ya ana kwa ana jioni ya jana, Jumatatu, Septemba 5, 2011, Ikulu, Dar es salaam.

Mwanamichezo huyo pia alimkabidhi Mheshimiwa Rais Kikwete jezi ya timu ya Whitecaps – Jezi Nambari Nne (04) – ikiashiria kuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ni Rais wanne wa Tanzania.

Katika mkutano wake na Mheshimiwa Rais, mwanasoka huyo aliandamana na wafadhili wengine wa soka akiwamo Bwana Rahim Kangezi na Bwana Robert Slavik ambaye pia ni Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za uchimbaji madini ya Ruby Creek Resources yenye shughuli zake katika wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi.
Katika mazungumzo hayo, Nizar Khalfan, mbali na kumshukuru Rais Kikwete na Serikali yake, pia amemwelezea kiongozi huyo kuhusu maendeleo yake ya soka katika medani ya soka ya kulipwa nchini Canada na matumaini yake ya baadaye.

“Mheshimiwa Rais, sasa Mungu ananisaidia kwa sababu napata nafasi zaidi ya kucheza katika timu yangu,” Nizar Khalfan alimwambia Mheshimiwa Rais na kuongeza kuwa shabaha na nia yake hasa ni kupata nafasi ya kucheza katika ligi kubwa na ngumu zaidi za Ulaya.”

No comments: