Wednesday, September 21, 2011

MAGONJWA YASIYO AMBUKIZI YANAONGEZA UMASKINI-TANZANIA


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani katika majadiliano ya kufatufa njia muafaka na zenye gharama nafuu za kuudhibiti na kutibu magonjwa yasiyo ambukizi.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete. Waziri wa Afya na maendeleo ya jamii kutoka Serikali ya mapinduzi Zanzibar, Mhe. Juma Duni Haji, amesema , magonjwa yasiyo ambukizi yanaendelea kuwa mzigo mkubwa hususani kwa familia maskini.
Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wamekutana kwa siku(jumatatu na jumanne) mbili kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu magonjwa manne ambayo si ambukizi. Magonjwa hayo ni Kansa, Kisukari, Ugonjwa wa Moyo na Ugonjwa wa Mapafu.
“Gharama za kutibu magonjwa haya ni mkubwa mno. Karibu kila familia ambayo imeathirika na moja ya magonjwa haya inatumia asilimia 40 ya kipato chao kugharamia matibabu. Haya ni magonjwa yanayosababisha familia nyingi kuwa maskini” akasema Waziri Duni ambaye ni kati ya mawaziri watatu walioambatana na Mhe. Rais Kikwete kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 66 wa Umoja wa Mataifa ambao unaanza siku ya jumatano..
Mkutano wa Kilele kuhusu magonjwa yasiyo ambukizi ni kati ya mikutano kadhaa ya kilele ambayo inafanyika kabla ya Mkutano Mkuu.
Kutoka na gharama kubwa ya kutibu magonjwa hayo, Waziri Juma Duni amesema, Tanzania inasisitiza umuhimu wa magonjwa hayo kuingizwa katika ajenda za Kimataifa za Maendeleo.
Akasisita kuwa ongezeko la magonjwa yasiyo ambukizi kumesababisha changamoto kubwa katika mfumo uliopo wa utoaji wa huduma za afya.
Akizungumzia uzoefu wa Tanzania , Waziri amesema serikali ilizindua mwaka 2009 mkakati wa kitaifa kuhusu magonjwa yasiyo ambukizi. Mkakati huo unalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya pamoja na utudhibiti wa magonjwa hayo.
Aidha akaainisha kwamba kama nchi, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili kwa pamoja. Changamoto hizo ni kukabiliana kwanza, na magonjwa yasiyo ambukizi na ya pili ni kukabiliana na magonjwa ambukizi.
Kutokana na changamozo hizo, Waziri Duni anasema kuwa si vema basi aina moja ya ugonjwa ikatiliwa mkazo na kupewa kipaumbele dhidi ya ugonjwa mwingine kwa kuwa yote yanashabihiana.
Aidha amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili Tanzania kuwa ni ongezeko la kansa ya shingo ya uzazi, ongezeko la wagonjwa wa kisukari wa asilimia tano, uvutaji wa sigara kwa asilimia 10, ongezeko la watu wenye utizo wa kupita kiasi, unywaji wa pombe na maelfu ya watoto wanaozaliwa wakiwa na matatizo ya sickle –cell kila mwaka.
Mwishoni wa Mkutano huo, viongozi wa kuu wa nchi na serikali walipitisha tamkio la kisiasa ambalo licha ya kukiri kwamba magonjwa hayo manne ni changamoto ya katika karne ya 21.Pia wamemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ( WHO)na wadau wengine kuandaa taarifa itakayowasilishwa kwa viongozi hao katika Mkutano Mkuu wa 67 wa Umoja wa Mataifa.
mwisho

No comments: