ATUHUMIWA KESI YA MELI WAPEWA DHAMANA BILA KUJUA TAREHE YA KWENDA TENA KORTINI


Watuhumiwa wa kesi ya mauajia ya meli ya Mv Spice iliyotokea Septemba 10 mwaka huu katika eneo la Nungwi Kisiwani Unguja Mjini Zanzibar na kuuwa watu zaidi ya 200,wakifikishwa Mahakama Kuu ya Zanzibar,wa mbele ni Nahodha Msaidizi wa meli hiyo Abdalla Moh'd Ali (30) katikati ni Yusufu Suleiman Jussa (47) ambaye ni mmiliki wa meli hiyo na mwisho ni Simai Nyange Simai (27) ni msimamizi wa bandari ya Malindi .Picha na Jackson Odoyo

****************************
Watuhumiwa watatu kati ya wanne waliofikishwa kwenye Mahakama Kuu Mjini Zanzibar wiki iliyopita wakikabiliwa na kosa la uzembe na kusababisha vifo vya watu 203 waliokuwa wakisafiri kwa Meli ya MV Spice Islander na kuzama katika bahari ya Hindi, Septemba 10 2011, wamepewa dhana na haikutaja siku ya kurejea tena Mahakamani hapo.

Watuhumiwa waliopewa dhamana ni Abdallah Mohammed Ali(30) mkazi wa Bububu, ambaye ni Afisa Mkuu wa Meli ya MV Spice Islander, Yussuf Suleiman Jussa(47), mkazi wa Kikwajuni ambaye pia ni Mmoja wa Wamiliki wa Meli na Msimamizi Mkuu wa Mizigo katika meli hiyo na Simai Nyange Simai(27) mkazi wa Mkele, ambaye ni Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mamlaka ya Usafiri Baharini anayehusika na usalama wa abiria melini.

Watuhumiwa hao, Ijumaa iliyopita walirejeshwa rumande baada ya kuzuka mabishano ya kisheria ya kutaka wapewe dhama ama wasipewe, ambapo Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru warejeshwe rumande hadi leo Jumatatu atakapotoa uwamuzi wake.

Walipofikishwa Mahakamani hapo hii leo, Wakili wa Utetezi Bw. Hamidi Ali Saidi Mbwezeleni aliiomba Mahakama iwaachie huru watuhumiwa hao ili tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza chanzo cha kuzama kwa meli hiyo iendelee na kazi yake la sivyo tume isitishe kazi yake hadi pale kesi itakapomalizika.

Wakili huyo amesema kuwa kutakuwa na utata kama watuhumiwa wataendelea kubaki rumande kwani watakosa haki yao ya msingi katika tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar wakati ikiendelea na kazi yake endepo itataka kupata taarifa ama maoni kutoka kwa watuhumiwa hao hivyo wakiwa mahabusu watakosa haki yao ya kujieleza mbele ya tume hiyo.

Amesema hivi sasa inaonekana kuna makundi mawili yanayofanya kazi moja kwa maana ya Mahakama na Tume jambo ambalo alisema litakuwa na utata na lenye makusudio ya kuwalinda baadhi ya watu fulani.


Comments